Bei ya nyama yapanda ghafla katika mji wa Bunazi Missenyi
4 January 2025, 2:38 pm
Na Respicius John, Missenyi Kagera
Baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Bunazi wilayani Missenyi wamelalamikia ongezeko la bei ya nyama ya ng’ombe iliyopanda holela kutoka shilingi elfu 8 mpaka shilingi elfu kumi kwa kipindi cha takribani miezi minne.
Wakiongea na Radio Karagwe FM kwa nyakati tofauti baadhi ya watumiaji wa nyama katika mji mdogo wa Bunazi wamelalamikia ongezeko hilo wakidai kuwa haliendani na uhalisia wa maisha yao na kipato chao. Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara ya nyama mjini hapo akiwemo Swidiq Mustafa wamedai kuwa kufungwa kwa minada ya ng’ombe na ongezeko la kodi wakati wa ununuzi wa ng’ombe kumechangia hali hiyo
Diwani wa kata ya Kasambya Yusuph Ahmada Mzumbe amekiri uwepo wa changamoto hiyo mjini Bunazi na kuahidi kufuatilia chanzo cha tatizo la upandishaji wa bei za kitoweo hicho
Kuhusu suala hilo kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi wakili Serafina Rwegasira ambaye pia ndiye mwanasheria wa halmashauri hiyo amesema kuwa halmashauri haina mamlaka ya kupanga bei ya bidhaa hiyo bali wafanyabiashara wenyewe hupanga bei kulingana na upatikanaji wa soko na bidhaa husika.
Pamoja na hayo amekanusha suala la kupanda ushuru kama lilivyotajwa na wafanyabiashara wa nyama akisisitiza kuwa viwango vya ushuru vilivyopo ni vya muda mrefu