Waliofariki ajali ya Karagwe watambuliwa, dereva atiwa mbaroni
4 December 2024, 9:37 pm
Miili ya watu watano kati ya saba waliofariki dunia kwa ajali iliyotokea Desemba 3,2024 katika kata ya Kihanga wilayani Karagwe imetambuliwa na kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa taratibu za mazishi
Na Jovinus Ezekiel
Serikali wilayani Karagwe imelitaka jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kuhakikisha linawachukulia hatua za kisheria baadhi ya madereva wanaoendesha vyombo vya moto pasipo kufuata sheria za usalama barabarani.
Akizungumuza wakati wa zoezi la kuaga miili ya marehemu waliopoteza maisha katika ajali ya Toyota Hiace iliyotokea hivi karibuni katika eneo la Kishoju kata ya Kihanga wilayani Karagwe, mkuu wa wilaya Karagwe Julius Laiser amewapa pole wanafamilia na wanakaragwe waliokusanyika katika kituo cha afya Kayanga ili kuaga miili ya marehemu hao Desemba 4, 2024 na kusema kuwa msiba huu ni funzo kwa waendesha vyombo vya moto kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani.
Amesema kuwa kwa sasa jeshi la polisi wilayani Karagwe kupitia kitengo cha usalama barabarani inabidi wawe makini katika kufuatalia na kuwachukulia hatua za kisheria madereva wote ambao hawafuati sheria za usalama barabarani.
Kwa uapande wake kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Kagera bw.Yassin Mwinori amesema kuwa majeruhi wote waliopokelewa katika hospitali ya mkoa Bukoba ambao ni wanane afya zao zinaendelea vizuri na kuwataka wananchi kutoa taarifa wanaposafiri kwa ndugu zao kwani baadhi ya majeruhi hawajapata ndugu zao huku mkuu wa polisi wilayani Karagwe Shaban Nyandular akisema kuwa dereva aliye sababisha ajali hiyo kwa sasa ameshakamatwa na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Hata hivyo katika miili ya marehemu saba miili minne imekabidhiwa kwa ndugu ili waendelee na taratibu za maziko ambapo mitatu kati ya hiyo ni ya familia moja.