Karagwe FM

Saba wapoteza maisha kwa ajali Karagwe

3 December 2024, 6:37 pm

Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Blasius Chatanda. Picha kwa hisani ya mtandao

Wimbi la ajali za barabarani linaendelea kuchukua uhai wa watu nchini Tanzania wanaotumia vyombo vya moto hususan magari ya abiria ambayo mara nyingi hugongana na magari ya mizigo

Na Shabani Ngarama

Watu saba wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa katikia ajali iliyohusisha magari matatu likiwemo lori la mizigo aina ya Scania, Toyota Hiace na Coaster eneo la beria ya ukaguzi katika kijiji na kata ya Kihanga wilayani Karagwe mkoani Kagera.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda amesema kuwa ajali hiyo imetokea Desemba 3, 2024 majira ya saa 5.00 asubuhi katika barabara ya Kihanga-Kyaka na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi na uzembe wa dereva.

Sauti ya kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Blasius Chatanda

Kamanda Chatanda ameongeza kuwa ajali hiyo imetokana na uzembe wa dereva ambaye kwa kiasi kikubwa anaonekana kuwa mgeni katika barabara hiyo na kwamba hakuchukua tahadhari kwenye eneo hilo lililokuwa likitumika kwa ukaguzi wakati anaingia beria

Sauti ya kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Blasius Chatanda

Hata hivyo kwa mujibu wa kamanda Chatanda dereva wa lori anayedaiwa kusababisha ajali na vifo hivyo amekimbia na jeshi la polisi linaendelea kumtafuta kwa ajili ya kumchukulia hatua za kisheria