Kagera yabuni mbinu kukomesha ukatili kwa wazee
7 October 2024, 10:03 pm
Baadhi ya zawadi zilizotolewa kwa wazee na Umoja wa amani kwanza. Picha na Theophilida Felician
Wazee ni tunu muhimu katika Jamii; wanapaswa kupokelewa, kuheshimiwa; wanateseka katika ukiwa, wanapotengwa na kuelemewa na upweke.
Na Theophilida Felician
Umoja wa amani kwanza mkoani Kagera umekemea vitendo vya kikatili dhidi ya wazee na kuitaka jamii kuendelea kuwajibika ipasavyo kwa kuwatunza na kuwalinda wazee ili kuwanusuru na changamoto zinazowakabili.
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa taasisi ya Umoja wa amani kwanza ndugu Mauldi Rashidi Kambuga alipoungana na wadau wa kundi la Kagera mpya na kwenda kuwafariji wazee wanaolelewa kituo cha Kiilima kilichopo kata ya Nyakato halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoa wa Kagera.
Mwenyekiti Kambuga awali ameanza kwa kuwatia moyo wazee hao huku akisisitiza kwamba wazee ni hazina na nikundi muhimu sana kwa jamii hivyo wanahitaji kuthaminiwa, kupendwa, kupewa faraja na mengineyo mengi ili kuwasadia kuishi vizuri kama ilivyo kwa makundi mengine.
Amesema kuwa wazee mara kadhaa wamekuwa wakikabiliwa na madhira mbalimbali yakiwemo ya ukatiri wa mauaji hivyo akaagiza matendo kutakiwa kukemewa kwa nguvu zote
Amewapongeza waliowaza nakuandaa zoezi hilo la kuwafikia wazee wa kilima huku akifafanua kwamba taasisi ya umoja wa amani kwanza baada ya kukabidhiwa wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee wanawake na watoto kutoka wizara ya mambo ya ndani imepata nguvu mpya yakuifikia jamii kwa kushiriki mambo tofauti tofauti likiwemo suala nyeti la kuhamasisha namna yakuitunza amani.
Viongozi wa dini sheikh Mussa Hassan pamoja naye Jovestus Sebastian katika dua wameelezea na kuhimiza jinsi wazee wanavyohitaji faraja ya kutunzwa vizuri hatimaye kuishi kwa neema badala ya kukatishwa tamaa kama ambavyo imekuwa ikijitokeza kwa baadhi ya wazee.
Mkuu wa mkoa Kagera Mhe Hajat Fatma Mwassa akiwa mgeni rasmi wakati akizikabidhi zawadi hizo kwa wazee ambazo ni nguo aina mbalimbali, sukari, mchele, unga, sabuni na viti mwendo amewapongeza wale wote kutoka kundi la Kagera mpya wakiongozwa na Jastin Kimodoi anayeishi Marekani aliyechochea jambo hilo kwa wenzake hadi likafanikiwa vyema.
Aidha ameipongeza taasisi ya umoja wa amani kwanza kwa namna ilivyojiimarisha na kuifikia jamii kisha kuitangaza injili ya amani kwani amani ndiyo inayowezesha kufanyika kwa kila jambo.