Rwamishenye wadai kuhujumiwa zawadi za ligi ya Byabato
18 September 2024, 8:16 pm
Baadhi ya wananchi wa kata ya Rwamishenye manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wameibuka na tuhuma dhidi ya diwani wa kata hiyo bw. Juma Sued Kagasheki wakimtuhumu kuhujumu zawadi walizostahili baada ya kuibuka na ushindi wa tatu katika mashindano ya ligi ya mbunge wa Bukoba mjini Stephen Byabato maarufu kama “Byabato Cup 2024“
Na Theophilida Felician.
Wananchi walioshiriki ligi ya Byabato CUP 2024 kata ya Rwamishenye manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wamemlalamikia diwani wa kata hiyo Juma Suedi Kagasheki kuhujuma ng’ombe waliyokabidhiwa kama zawadi baada ya kupata ushindi katika ligi hiyo.
Baadhi ya wadau wakiongozwa na Evodius Rugemalila wakizungumza na vyombo vya habari eneo la kata ya Rwamishenye wamesema kuwa katika ligi hiyo wao walipata nafasi ya tatu ambayo zawadi zao ni fedha kiasi cha shilingi milioni moja na ng’ombe ambavyo kwa pamoja vilikabidhiwa kwa diwani huyo katika viwanja vya Kaitaba takribani mwezi mmoja na nusu umepita tangu kukamilika kwa ligi na hawajapata chochote.
Wamemtaka diwani huyo kujitokeza hadharani kuelezea ni wapi zawadi hizo zilipo ili waweze kufanya sherehe kama walivyokwisha fanya kwa washindi wa kata nyingine vinginevyo watapiga hatua zaidi ili kuhakikisha haki yao inapatikana kwani tayari wana taarifa za kuaminika kuwa ng’ombe huyo alishauzwa kimyakimya.
Hata hivyo diwani juma Suedi Kagasheki amekanusha tuhuma dhidi yake akisema kuwa hahusiki na suala hilo.