Karagwe FM

RC Kagera asisitiza kuwaenzi mashujaa kwa kudumisha amani

26 July 2024, 2:48 pm

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwasa akihutubia kwenye kumbukumbu ya mashujaa Julai 25, 2024. Picha na Theophilida Felician

Kila ifikapo Julai 25, Tanzania huadhimisha kumbukizi ya mashujaa waliopigania uhuru wa taifa hili ambapo kwa mwaka 2024 maadhimisho haya yamefanyika jijini Dodoma kitaifa yakiongozwa na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.

Theophilida Felician.

Mkoa Kagera umeungana na wananchi wengine hapa nchini kushiriki siku ya kumbukumbu ya mashujaa waliopambana na wanaoendelea kupambana ili amani ya nchi iendelee kuwa tulivu kama ilivyo kwa kipindi chote.

Akishiriki maadhisho hayo Tarehe 25 Julai 2024 mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwasa katika viwanja vya uhuru Mayunga Manispaa ya Bukoba amesema kuwa siyo kazi ndogo kuidumisha amani kwa miaka mingi hivyo ni muhimu watu wote kuwakumbuka mashujaa kwa kudumisha amani na utulivu.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwasa
Mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwasa akiweka ngao kwenye ngao kwenye mnara wa mashujaa Mayunga manispaa ya Bukoba. Picha na Theophilida Felician

Mkuu wa mkoa Mwasa amepewa heshima ya kuweka ngao kwenye mnara wa mashujaa Mayunga hivyo ameahidi kufanya jitihada za kulikarabati eneo hilo ili kuendelea kuweka sawa kumbukumbu za mashujaa hao.

Hata hivyo baadhi ya viongozi akiwemo kiongozi wa JWTZ Mkoa wa Kagera Luteni Kanali Nimrod Ezekiel ambaye ameweka sime kwenye mnara huo akifuatiwa na viongozi wa dini walioweka mashada wamewaombea pumziko jema mashujaa waliokwishatangulia mbele ya haki huku wakiwatakia kheri na afya njema ambao wanaendelea na majukumu ya kulilinda Taifa akiwemo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Luteni Kanali Nimrod Ezekiel akiwakilisha wanajeshi kuweka Sime kama ishara ya kuwakumbuka mashujaa waliotangulia mbele ya haki

Nao baadhi ya mashujaa wa vita ya Kagera wamepewa nafasi ya kusalimia nakuyaelezea mambo kadhaa jinsi walivyopigana hadi kumfurusha Iddi Amini na majeshi yake.

Baadhi ya mashujaa wa vita vya Kagera walioshiriki kumbukumbu ya mashujaa Julai 25.2024. Picha na Theophilida Felician

Hata hivyo wametoa wito wakiwasihi askari ambao wako katika majukumu kufanya kazi zao kwa kutanguliza moyo wa kulipenda Taifa huku wakiipongeza serikali ya mkoa kwa namna ilivyowatambua na kuwashirikisha katika tukio hilo muhimu.

Sauti ya baadhi ya mashujaa wakisimulia waliyoyapitia wakati wa vitaa vya Kagera
Baadhi ya viongozi wa dini wakiweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu ya mashujaa. Picha na Theophilida Felician