Karagwe FM

WEO Kanyigo asusiwa kikao kwa kufukuza wanahabari

12 July 2024, 3:30 pm

Baadhi ya wajumbe waliosusia kikao. Picha na Theophilida Felician

Wandishi wa habari nchini wanaendelea kukumbana na vikwazo kazini kila uchao licha ya matamko yanayotolewa na viongozi wa kitaifa katika majukwaa mbalimbali. Ni hivi karibuni tu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika kilele cha siku ya uhuru wa vyombo vya habari Mei 3, 2024 alisisitiza watendaji wa serikali kutoa ushirikiano kwa wanahabari ili wapate na kuripoti matukio kwa usahihi.

Na Theophilida Felician.

Wadau wa maji kata ya Kanyigo halmashauri ya Missenyi mkoani Kagera wamevunja kikao ghafla cha bodi ya maji kilichokuwa kimeandaliwa na bodi ya maji ya wilaya na kufanyika shule ya sekondari Kanyigo Muslim Seminary tarehe 11 Julai 2024 kutokana na afisa mtendaji wa kata hiyo Bw. Daudi Kyaka kutoa tamko la amri ya kuwaondoa kwenye kikao waandishi wa habari wawili waliokuwa wamealikwa na bodi hiyo ya maji kutoka Radio Karagwe na Kasibante kushiriki kikao hicho.

Hali hiyo imetokea muda mfupi baada ya kuanza kwa kikao ambapo afisa huyo alisimama na kutoa amri hiyo akidai kwamba maagizo hayo amepewa na mkuu wa wilaya ya Missenyi Kanali mstaafu Hamis Mayamba Maiga.

Tamko hilo wananchi hawakuwa tayari kukubaliana nalo huku wakimuhoji kwanini anawafukuza wandishi wa habari?

Sauti ya mtendaji wa kata ya Kanyigo bw Daudi Kyaka na wananchi waliopinga kauli yake

Kutokana na sintofahamu hiyo iliyojitokeza muda mfupi kuanza kwa kikao na kuwasili kwa watumishi wa wakala ya usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA wilaya ya Missenyi wadau wakachukua maamuzi ya kutoka ndani ya ukumbi na kutawanyika wakiashiria kutokukubali kitendo kilichotekelezwa na mtendaji huyo.

Baadhi ya wajumbe walioongea na wandishi wa habari nje ya ukumbi kulalamikia mtendaji kufukuza wanahabari. Picha na Theophilida Felician

Baadhi ya wadau baada ya kutawanyika wameelezea kusikitishwa na kitendo hicho ambapo wameomba serikali kushughulikia suala hilo kwani halina nia njema katika ujenzi wa maendeleo ya wananchi.

Wameongeza kwamba mradi wa Kanyigo umekuwa na changamoto mbalimbali zinazopelekea wananchi kutokupata maji kwa ufasaha.

Sauti ya wajumbe wa bodi ya maji Kanyigo wakieleza kukerwa na kilichotokea kwenye mkutano

Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Missenyi kanali mstaafu Hamis Mayamba Maiga akizungumza kwa njia ya simu amekanusha kuhusika na agizo hilo.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Missenyi kanali msataafu Hamis Maiga akikanusha kuhusika na kuagiza wandishi kufukuzwa

Haya yanajiri miezi michache tangu waziri mkuu Kassim Majaliwa alipowataka viongozi na watendaji wa Serikali waondoe ukiritimba kwenye suala la upatikanaji wa habari ili kuwawezesha wanahabari kupata taarifa sahihi na kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Alitoa wito huo Ijumaa, Mei 3, 2024 wakati akizungumza na wanahabari na wadau wengine kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Sauti ya waziri mkuu Kassim Majaliwa akiwaasa wakuu wa taasisi na watendaji serikali kuondoa ukiritimba wa upatikanaji wa habari