Karagwe FM

Waziri Bashungwa awaita wawekezaji kuja Karagwe

8 July 2024, 7:38 pm

Waziri wa ujenzi na mbunge wa jimbo la Karagwe Innocent Bashungwa akimpongeza diwani wa kata ya Bugene Mugisha Anselmi kwa uwekezaji wa hoteli ya Mlimani City Mikyolo. Picha na Eliud Rwechungura

Sekta ya uwekezaji hutegemea mazingira ya eneo husika na uhitaji wa soko la bidhaa zitakazopatikana kutokana na uwekezaji husika. Kwa wilaya ya Karagwe mazingira ya uwekezaji yako vizuri licha ya changamoto ndogo ya miundombinu ya maji na barabara ambazo mbunge wa jimbo la Karagwe na waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa anazishughulikia kwa kadri ya uwezo wake.

Na mwandishi wetu

Waziri wa ujenzi, Innocent Bashungwa na mbunge wa jimbo la Karagwe mkoani Kagera ameeleza kuwa serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha miundombunu ya barabara katika wilaya ya Karagwe hivyo amewataka wawekezaji na Wafanyabishara kuendelea kuchangamkia fursa za uwekezaji.

Bashungwa ameeleza hayo leo Julai 07, 2024 wakati akizundua hoteli mpya ya Mlimani City Mikyolo iliyopo kata ya Bugene, wilaya ya Karagwe na kueleza kuwa  serikali inaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi ili kuwezesha wawekezaji kuwekeza na kuzalisha ajira mbalimbali kwa watanzania.

“Tunajionea jinsi wilaya ya Karagwe inavyoendelea kukua kila siku hususani katika miundombinu ya barabara, kama mnavyofahamu kazi za ujenzi wa barabara ya Bugene – Nyaishozi kuelekea Benaco inaendelea kwa kasi, sambamba na hiyo tumeshampata mkandarasi wa kuanza ujenzi wa barabara ya Omurushaka – Kyerwa kwa kiwango cha lami” ameeleza Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa barabara zinazojengwa zikikamilika zitasaidia wilaya ya Karagwe kufungua fursa za kibiashara ambazo zitawezesha wananchi kutumia nafasi hiyo kukuza uchumi wao binafsi na pato la taifa.

Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa uongozi wa Hoteli ya Mlimani City Mikyolo kutoa huduma bora na nzuri kwa wateja wake ili kuwavutia wateja wengine ambao wataeneza sifa nzuri za hoteli hiyo pamoja na ukarimu wa wanakaragwe.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Bw. Wallace Mashanda akisisitiza jambo mbele ya Mbunge na waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa. Picha na Eliud Rwechungura

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe, Wallace Mashanda ameeleza kuwa uwekezaji katika wilaya ya Karagwe ni muhimu sana kwani wilaya hiyo imepakana na hifadhi na mbuga za wanyama za Burigi -Chato na Ibanda Kyerwa, hivyo uwepo wa hoteli utaongeza idadi ya wataliii kufika na kutembelea hifadhi hizo.

Kwa upande wake, diwani wa kata ya Bugene, Mugisha Anselmi amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo ambapo amewapatia shilingi milioni 580 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Omurushaka na kiasi cha shilingi milioni 260 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya shule ya sekondari ya Bugene.

Bw. Ezekia Anselmi akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Mbunge wa jimbo la Karagwe na waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa. Picha na Eliud Rwechungura

Akisoma Risala ya Uzinduzi, Bw. Ezekia Anselmu ameeleza kuwa hoteli ya Mlimani City Mikyolo ina vyumba vya kulala vyenye hadhi ya juu, eneo la maegesho ya magari lenye usalama wa kutosha, bustani za kupumzikia na viunga vyenye hewa safi na tulivu.