Ujenzi wa lami ya Bugene hadi Kyerwa kuanza hivi karibuni
8 July 2024, 6:35 pm
Katika maeneo ambayo wananchi wamekuwa na kilio cha ubovu wa miundombinu mibovu ya barabara na kuwa uhitaji mkubwa wa barabara ya lami ni wilaya ya Kyerwa hasa barabara ya kuanzia Bugene kwenda Kyerwa kupitia mji wa Nkwenda. Hakika barabara hii ni muhimu kwa wananchi kwani inaunganisha wilaya hizi mbili ambazo zamani ilikuwa wilaya moja ya Karagwe
Na mwandishi wetu
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa serikali kupitia Wakala wa barabara nchini (TANROADS) imeshampata mkandarasi wa kuanza ujenzi wa barabara ya Omurushaka – Kyerwa kwa kiwango cha lami ambapo hivi karibuni atamleta mkandarasi aliyepewa kazi hiyo kumtambulisha na kumkabidhi kwa wananchi ili kuanza ujenzi.
Ameeleza hayo katika mkutano wa hadhara wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Ihanda mwishoni mwa wiki na kueleza kuwa tayari mkandarasi ameshaoneshwa eneo la kujenga kambi na kupima maeneo mawili ya Ihanda wilaya ya Karagwe na Nkwenda kwa upande wa wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Bashungwa amefafanua kuwa barabara ya Omurushaka – Kyerwa itaunganisha nchi ya Tanzania na Uganda kupitia mpaka wa Murongo na itapita kwenye wilaya mbili za Karagwe na Kyerwa hivyo ni barabara muhimu kiuchumi kwa kuwa inapita maeneo muhimu yenye uzalishaji mwingi wa kahawa, ndizi maharage ambapo wananchi watanufaika nayo.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashungwa amechangia kiasi cha shilingi Milioni 12 ili kukamilisha ujenzi wa jengo la zahanati ya kata ya Ihanda na kusisitiza kuwa kazi zingine zilizobakia ziendelee ili kufikia mwaka 2025 zahanati ianze kutoa huduma kwa wananchi wa kata hiyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ihanda, Ladislaus Kamuhangire ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa zahanati ya Ihanda ulianza mwezi Machi, 2023 ambapo hadi hivi sasa umefikia hatua ya kuezeka na ikikamilika itasaidia kutatua changamoto ya umbali wa upatikanaji wa huduma ya afya kwa wananchi wa kata hiyo kuzifikia kituo cha afya cha Kayanga na Hospitali ya wilaya ya Karagwe Nyakanongo ambapo hata hivyo Bashungwa ameahidi kuchangia ujenzi huo.