Karagwe FM

Moto wa ajabu wateketeza nyumba tano Bunazi Missenyi

27 June 2024, 7:42 pm

Moja ya nyumba zilizoteketezwa na moto wa maajabu Bunazi Missenyi. Picha na Respicius John

Na Respicius John

Wakazi wa mji mdogo wa Bunazi kata ya Kassambya wilayani Missenyi mkoani Kagera wameiomba serikali kuchunguza chanzo cha moto unaoripuka katika mazingira ya kutatanisha na kuunguza nyumba za watu katika kitongoji cha Bunazi B

Wakiongea na waandishi wa habari baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Bunazi B wamesema kwamba katika mtaa wao tangu tarehe 14/06/2024 jumla ya nyumba tano zimeungua moto likiwemo bweni la wasichana katika shule ya sekondari Bunazi

Familia iliyounguliwa makazi katika mji mdogo wa Bunazi wilayani Missenyi. Picha na Respicius John

Mmoja kati ya watu waliounguliwa na nyumba yake na kupoteza vitu vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni nane bw. John Gabriel amesema kuwa hajui chanzo cha moto ulioteketeza nyumba yake huku akiomba serikali imsaidie huduma za kibinadamu na mahali pa kuishi na kwamba kwa sasa analala nje ya nyumba ya jirani yake

Sauti ya baadhi ya wananchi waliokumbwa na adha ya kuunguliwa nyumba zao kimiujiza

Mwingine aliyeunguliwa nyumba yake ni kiongozi wa dini Katekista Adeltus Joseph ambaye amesema kuwa hawajui chanzo cha moto kwani unaripuka mchana kimiujiza huku akiomba serikali iwasaidie mahali pa kulala pamoja na kudhibiti moto unaoendelea kwenye kitongoji chao

Kaimu kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Kagera mrakibu mwandamizi George Mrutu amethibitisha kuwepo kwa moto huo na kwamba wanaendelea na uchunguzi wa kina kwa sababu vyanzo vyake ni vya sintofahamu

Sauti ya kiongozi wa dini Katekista Adeltus Joseph pamoja na Kaimu kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Kagera mrakibu mwandamizi George Mrutu

“Tumewaachia wanakijiji pamoja na serikali ya wilaya ya Missenyi kulishughulikia sababu moto unaoripuka siyo kwamba umewashwa, godoro na matandiko vinaungua mpaka vinaisha lakini kitanda cha mbao hakiungui kabisa,unachoma chumba kimoja unaruka na kwenda chumba kingine unaunguza vitu lakini nyumba haiteketei kwahiyo wanajamii wakae ili kubaini sintofahamu” Amesema kamanda Mrutu

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Missenyi kanali mstaafu Hamis Mayamba Maiga amesema kwamba wanasubiri taarifa kutoka jeshi la zimamoto ili ifanyiwe kazi na kwamba Jumatatu Juni 27 atakutana na wahanga wa moto huo ili kuona jinsi ya kuwasaidia huku diwani wa kata ya Kassambya Yusuf Mzumbe akisema kwamba wamepanga kushirikiana na viongozi wa dini kufanya maombi maalum kwa ajili ya jambo hilo

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Missenyi kanali mstaafu Hamis Mayamba Maiga