Karagwe FM

Matukio ya ukatili kwa watoto yafikia 729 Karagwe

18 June 2024, 9:54 pm

Baadhi ya washiriki wa sherehe za siku ya mtoto wa Afrika. Picha na Ospicia Didace

Siku ya Mtoto wa Afrika, ni siku inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 16 Juni tangu mwaka 1991, ilipoteuliwa na Umoja wa Afrika (AU) katika kuenzi michango ya watoto walioshiriki katika maandamano kwenye mji wa Soweto nchini Afrika Kusini mnamo mwaka 1976 pamoja na kujengea jamii uelewa juu ya umuhimu wa elimu bora kwa watoto wote.

Na Ospicia Didace

Wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera imeripoti ongezeko la vitendo vya ukatili kwa watoto kwa kuwa na jumla ya matukio 729 yaliyoripotiwa kwa jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia kwa kipindi cha mwaka 2023/2024.

Kupitia maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyoadhimishwa wilayani Karagwe mwaka 2024 chini ya kauli mbiu “Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi”, Mkaguzi Msaidizi wa polisi wilayani Karagwe Zaina Waziri amewaasa wazazi na jamii kwa ujumla kushirikiana katika ulinzi wa mtoto kwa kutenga muda wa kuzungumza na watoto na kufahamu changamo wanazopitia ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili.

Sauti ya mkaguzi msaidizi wa polisi wilaya ya Karagwe Zaina Waziri

Editha Athanas ni mwanafunzi wa shule ya sekondari Bushangaro aliyesoma risala kwa niaba ya kamati ya maandalizi ya sherehe hiyo mbele ya mgeni rasmi katibu tawala wa wilaya ya Karagwe Rasul Shandala aliyemwakilisha mkuu wa wilaya iliyoeleza ongezeko la vitendo vya ukatili kwa mwaka 2024 ukilinganisha na mwaka 2023 na kuwa matukio yaliyofikishwa mahakamani ni 84 na matukio 40 tayari yamehukumiwa.

Alisema kuwa matukio ya ukatili wa kimwili yalikuwa 65 mwaka 2023 na mwaka 2024 kufikia mwezi Mei matukio 58 na kufanya jumla ya matukio 123 wavulana wakiwa 55 na wasichana 68. Aliongeza kuwa kati ya matukio hayo ni matukio matano yaliyohukumiwa kati ya kesi 7 zilizofikishwa mahakamani na kwamba ukatili wa kihisia pia unaongezeka.

Sauti ya mwanafunzi wa shule ya sekondari Bushangaro wilayani Karagwe Editha Athanas
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Wallace Mashanda. Picha na Ospicia Didace

Serikali inalo jukumu kubwa la kukemea kwa nguvu zote vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa mtoto kudhalilishwa kama alivyobainisha mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Wallance Mashanda kwamba kupitia baraza la madiwani walipendekeza kuongezwa bajeti katika ofisi ya ustawi wa jamii ili kuwezesha ofisi hiyo kupinga vita vitendo vya kiukatili katika maeneo mbalimbali.

Sauti ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Wallace Mashanda.
Katibu tawala wilaya ya Karagwe Rasul Eliud Shandala (aliyesimama) akiongea na wananchi. Picha na Ospicia Didace

Kwa upande wake mgeni rasmi katibu tawala wa wilaya ya Karagwe Rasul Shandala kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Laiser kwenye maadhimisha hayo yaliyofanyika katika kijiji cha Nyakagoyegoye kata ya Kiruruma amesema changamoto zinazowakumba watoto zinachagizwa na wazazi wasiotimiza wajibu wao katika malezi huku akieleza kusikitishwa na ongezeko la vitendo vya ubakaji na ulawiti ukilinganisha na mwaka 2023

Sauti ya Katibu tawala wilaya ya Karagwe Rasul Eliud Shandala