DC Karagwe atengua maamuzi ya kijiji kugawa ardhi
16 June 2024, 9:31 pm
Mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Kalanga Laiser ameendeleza utaratibu wa kuwasikiliza wananchi wa kata mbalimbali wilayani hapa ili kupunguza baadhi ya kero zilizopo ndani ya uwezo wake. Awamu hii aliwafikia wananchi wa kata za Kiruruma na Kamagambo na kusikiliza kero zinazowasibu.
Na Jovinus Ezekiel
Wananchi wa kata za Kiruruma na Kamagambo wilayani Karagwe mkoani Kagera wameeleza kuwepo kwa baadhi ya vifo vitokanavyo na matukio ya watu kujinyonga kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kusumbuliwa na madalali wa kahawa walioingia makubaliano na wakulima kununua kahawa mbichi mashambani.
Hili limeelezwa na baadhi ya wananchi wa kata hizo wakiwemo bw.Kafulika Elick na Merchades Tito ambao wamesema kuwa changamoto hiyo inatokana na madalali kuingia makubaliano ya utapeli na wakulima wakati kahawa zikiwa shambani na zinapostawi wanaingia kuvuna tofauti na makubaliano ya awali ambapo hata hivyo mkuu wa wilaya amekemea biashara ya kahawa zikiwa mashambani na kuwataka wakulia kutoa taarifa juu ya madalali wasiofuata utaratibu
Kero nyingine ambayo mkuu wa wilaya Karagwe bw, Laizer aliikuta katika kijiji cha Nyakagoyagoye kata ya Kiruruma ni migogoro ya ardhi baina ya wananchi na serikali ya kijiji hicho iliyoelezwa na bw, Elias Kyaluenda aliyedai kuwa ardhi yake ilichukuliwa huku mkuu wa wilaya akimtaka afisa mtendaji wa kijiji cha Nyakagoyagoye bw.Nelson Kahendaguza kutoa majibu kuhusu ardhi hiyo ambayo hata hivyo hayakumridhisha
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya alilazimika kubatilisha maamuzi ya serikali ya kijiji hadi utakapofanyika uchaguzi wa mwenyekiti wa kijiji kwa kuwa maamuzi yaliyofanyika awali hayakufuata utaratibu
Pamoja na changamoto zilizopo katika baadhi ya maeneo ya kata ya Kiruruma, diwani wa kata hiyo bw. Evarister Sylvester ameishukuru serikali kwa kutoa shilingi milioni 189.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu na kwamba kwa sasa wapo wanaezeka vyumba vya madarasa ikiwa ni baada ya kupokelewa fedha hiyo kwenye akaunti ya shule