Vijana watakiwa kushiriki mapambano ya rushwa Missenyi
1 June 2024, 6:42 pm
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU nchini imeendelea na kampeni za kudhibiti vitendo vya kutoa na kupokea rushwa kwa kutumia makundi ya vijana katika shule za sekondari maarufu kama klabu za wapinga rushwa
Na Respicius John
Vijana wanaoendelea na masomo katika shule mbalimbali za sekondari wilayani Missenyi mkoani Kagera wametakiwa kushirikiana na jamii katika vita dhidi ya rushwa na biashara ya dawa za kulevya ili kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa haki.
Wito huo umetolewa na mkuu wa wilaya ya Missenyi mkoani Kagera kanali mstaafu Hamis Mayamba Maiga katika tamasha la klabu za vijana wapinga rushwa kutoka shule mbalimbali za sekondari wilayani humo lililofanyika katika uwanja wa mashujaa Bunazi na kueleza kuwa vitendo vya rushwa hudumaza haki za watu na kuongeza mzunguko wa biashara ya dawa za kulevya kwa vijana wenye tamaa ya mali
Akiongea kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Missenyi mkuu wa divisheni ya kilimo, mifugo na uvuvi bi Tapita Tuvana Solomoni ameipongeza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini TAKUKURU kwa kutoa mafunzo kwa vijana juu ya madhara ya rushwa akisema kuwa kufanya hivyo kutaokoa kizazi kijacho ambapo hata hivyo vijana walitaja baadhi ya madhara ya rushwa katika jamii
Tamasha la klabu za wapinga rushwa wilayani Missenyi limeratibiwa na TAKUKURU wilayani humo ambapo afisa wa taasisi hiyo bw. Sospeter Joseph amewataka wananchi wote kutoa ushirikiano TAKUKURU ili kuiwezesha kupambana na rushwa katika jamii