Karagwe FM

Maji moto Mutagata Kyerwa yaripotiwa kutibu maradhi mbalimbali

29 May 2024, 6:05 pm

Mwangalizi wa eneo la maji moto Mutagata kijiji cha Rwabigaga kata ya Kamuli wilayani Kyerwa mkoani Kagera Mzee Angelo Mathias. Picha na Ramadhan Kassim

Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye vivutio vya utalii ambavyo havijajulikana kutokana na mkoa huu kuwa pembezoni. Chanzo cha maji moto Mutagata kilichopo katika kijiji cha Rwabigaga kata ya Kamuli kimekuwa kivutio cha utalii kwa wakazi wa mkoa huu kikiwa na historia ya maji yake kutumika kama tiba ya maradhi mbalimbali na kuondoa mikosi kwa anayeoga maji hayo

Na Catus Tito Kato

Wananchi mkoani Kagera na watanzania kwa ujumla wametakiwa kutembelea vyanzo vya utalii vilivyopo mkoani hapa kikiwemo chanzo cha maji moto Mutagata kilichoko kata ya Kamuli wilayani Kyerwa ili kujionea maajabu yaliyopo na faida zake.

Akiongea na baadhi ya wandishi wa habari mkoani Kagera waliofika kwenye chanzo cha maji moto Mutagata mwenyekiti wa kijiji cha Rabigaga kata ya Kamuli Julius Rwabigaga amesema kuwa yeye ni shahidi kwa watu waliotumia maji moto Mutagata na kupona magonjwa waliyokuwa nayo na kutoa wito kwa watanzania kufika eneo hilo kujionea maajabu

Sauti ya mwenyekiti wa kijiji cha Rwabigaga Julius Rwechungura akieleza juu ya ponyo litokanalo na maji moto Mutagata
Mwenyekiti wa klabu ya wandishi wa habari mkoa wa Kagera bw. Mbeki Mbeki (mwenye vazi la UTPC) akiwa na baadhi ya wandishi na wadau waliofika kwenye chanzo cha maji moto Mutagata hivi karibuni. Picha na na Ramadhan Kassim.

Mwenyekiti wa klabu ya wandishi wa habari mkoa wa Kagera bw. Mbeki Mbeki aliyeratibu safari ya wandishi wa habari mkoa wa Kagera akishirikisha wanafunzi wa chuo chake kijulikanacho kama Perfect Education and Training Institute (PETI) amesema kuwa wamefika katika chanzo hicho ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Tanzania, The Royal Tour katika kuutangaza utalii wa Kagera ili watu wa maeneo mengine wajue chanzo hiki kupitia vyombo vya habari. Hata hivyo mmoja wa wanahabari walioshiriki utalii huu wa ndani ni Afisa habari wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe bi Merabu Bilakashekwa anayebainisha mambo yasiyofahamika kuhusu maji moto Mutagata.

Baadhi ya wandishi na wadau waliotembelea chanzo cha maji moto Mutagata. Picha na Ramadhan Kassim

Naye diwani wa kata ya Kamuli aliyeambatana na wanahabari na wanafunzi wa chuo cha PETI cha Kayanga wilayani Karagwe amesema kuwa serikali kupitia baraza la madiwani wameweka mpango wa kutunza chanzo hicho kwa kujenga uzio ili kisiharibiwe na wananchi wanaoishi katika maeneo ya karibu

Diwani wa kata ya Kamuli wilayani Kyerwa Jonas Vedasto akielezea namna ya kutengeneza zana za ngozi kwa kutumia kifaa alicho nacho mkononi. Picha na Ramadhan Kassim
Sauti ya diwani wa kata ya Kamuli Jonas Vedasto