Karagwe FM

Magendo yatishia ukosefu wa kahawa Missenyi

10 May 2024, 8:08 pm

Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi Willy Mutayoba. Picha na Salimu Ramadhan

Suala la magendo ya kahawa mkoani Kagera limekuwa suala mtambuka kila inapofika nyakati za uvunaji wa zao hilo ambapo wakulima wengi wanadaiwa kuuza maua au kuvuna kahawa mbichi na kuuza kwa njia ya magendo hasa wakulima wanaopakana na nchi ya Uganda wanakodai kuwa kuna bei nzuri kuliko Tanzania

Na Shabani Ngarama.

Baadhi ya madiwani wilayani Missenyi mkoani Kagera wameingiwa na hofu ya kukosekana kwa kahawa katika msimu wa 2024/2025 kutokana na ongezeko la magendo ya kahawa inayosafirishwa na kuuzwa nchi jirani ya Uganda ikihusisha pia uvunaji wa kahawa mbichi wilayani humo.

Hoja hii iliibuliwa siku ya kwanza ya kikao Mei 9, 2024 na madiwani wakati wa kikao cha robo ya tatu kilichoongozwa na makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi bw. Willy Mutayoba aliyepokea maoni ya madiwani wanaolalamikia ongezeko la magendo ya kahawa na kwamba wanapoelekea watashindwa kudhibiti hali hiyo na kusababisha ukosefu wa zao hilo msimu utakapoanza rasmi.

Bw. Mutayoba akalazimika kuwatoa hofu madiwani akisema kuwa serikali haiwezi kushindwa kudhibiti magendo na kuiagiza serikali kutumia vyombo vya ulinzi na usalama na kuchukua hatua kunusuru zao hilo.

Sauti ya makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi bw. Willy Mutayoba
Makamu mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Kagera (KCU 1990 Ltd) bw. Respicius John akihutubia madiwani wilayani Missenyi. Picha na Salimu Ramadhan

Hata hivyo baraza la madiwani wilaya ya Missenyi lilitoa mwaliko kwa uongozi wa chama kikuu cha ushirika Kagera KCU 1990 Ltd katika kikao cha siku ya pili Mei 10, 2024 ili kupata mwelekeo wa soko la kahawa msimu huu ambapo katika taarifa ya KCU iliyotolewa na makamu mwenyekiti wa ushirika huo bw. Respicius John amekiri kuwepo kwa biashara ya magendo na wizi wa kahawa kutokana na ongezeko la bei na kulishauri baraza la madiwani kudhibiti hali hiyo.

Sauti ya makamu mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Kagera (KCU 1990 Ltd) bw. Respicius John
Baadhi ya madiwani wa Missenyi wakiwa katika kikao. Picha na Salimu Ramadhan

Wakichangia taarifa yake baadhi ya madiwani akiwemo Msafiri Nyema wa kata ya Ishunju na Rafiu Abeid wa kata ya Ruzinga wakaishukuru KCU kwa ongezeko la bei ya kahawa msimu uliopita na kutoa angalizo la ongezeko la magendo ya zao hilo kwa msimu mpya utakaoanza hivi karibuni

Sauti ya diwani wa kata ya Ishunju Msafiri Nyema na Rafiu Abeid, diwani wa kata ya Ruzinga

Akijibu baadhi ya hoja za madiwani bw. John amesema kuwa kwa msimu mpya wakulima wataruhusiwa kupanga bei wenyewe na kuuza kwa chama cha msingi kinacholipa bei kubwa kulingana na ubora wa zao hilo na kuwaasa wakulima kuhakikisha mibuni yao inakuwa na ubora na kuvuna kahawa zilizoiva na kuzianika vizuri

Sauti ya makamu mwenyekiti wa KCU bw. Respicius John akijibu hoja za madiwani