Bei ya nguruwe yasababisha kifo
1 May 2024, 8:40 pm
Nchi sita kati ya kumi zenye idadi kubwa kabisa ya watu kujiua duniani ziko Afrika, na kiwango cha kujiua katika bara hilo ni zaidi ya moja ya tano ikilinganishwa na maeneo mengine, WHO imesema wiki hii.
Na Devid Geofrey:
Mtu aliyefahamika kwa jina la Jackson Clemence Rwamuyonga mkazi wa kitongoji Mushasha kijiji Ruhanya kata ya Chanika wilaya ya Karagwe mkoani Kagera amejiua kwa kunywa sumu ya magugu baada ya kutofautiana bei ya shilingi Elfu 50 ili kumuuza Nguruwe.
Tukio hilo limetokea April 29, 2024 ambapo mwanaume aliyejulikana kwa majina ya Jackson Clemence Rwamuyonga alijiua kwa kunywa sumu ya magugu inayoitwa paraforce baada ya kutofautiana na mke wake bei ya kumuuza nguruwe ambapo alikusudia kumuuza laki moja na elfu hamsini huku mke wake akihitaji auzwe kwa shilingi laki mbili.
Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi ya mwanaume huyo katika kata ya Chanika wilaya ya Karagwe, diwani wa kata hiyo bw. Longino Wilbard amekemea vitendo vya mauaji kwa kutumia sumu ambapo amesema kuanzia Januari, 2023 hadi Aprili 2024 zaidi ya watu 20 wawili wakiwa wanawake wameripotiwa kufa kwa kunywa sumu na wengine kuuawa kikatili.
Naye katibu wa kitongoji hicho kwa niaba ya mwenyekiti wa kitongoji hicho amesema marehemu ameacha mke mmoja, watoto wanne na kwamba tukio hilo ni la pili katika kitongoji hicho la watu kujiua kwa kunywa dawa ya magugu.
Kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Kagera Blasius Chatanda amekemea tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi na akawataka kutafuta msaada kwa jeshi la polisi, viongozi wa dini na hata kwa viongozi wa serikali.
Mwili wa marehemu Jackson Clemence Rwamuyonga umepumzishwa nyumbani kwao kitongoji Mushasha kijiji Ruhanya kata ya Chanika wilaya ya Karagwe April 30 mwaka huu.