Wananchi wapewa mbinu za kukomesha uhalifu
22 April 2024, 8:43 am
Jamii bila uhalifu inawezekana ikiwa ushirikiano na utoaji wa taarifa kwa wakati kwa jeshi la polisi vitapewa kipaumbele.
Na Eliud Henry:
Wananchi wilayani Karagwe wametakiwa kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kuripoti vitendo vya kihalifu ili kudumisha amani katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na mkuu wa jeshi la polisi wilayani Karagwe mkoani Kagera Abdallah Shabani Nyandular hivi karibuni katika mkutano wa mkuu wa wilaya ya Karagwe kusikiliza na kutatua kero za wananchi uliofanyika katika tarafa ya Nyaishozi wilayani Karagwe.
Akitoa majibu kuhusu kero ya uhalifu unaofanyika katika mji mdogo wa Nyaishozi OCD Nyandular amesema kuwa jeshi la polisi wilayani Karagwe kwa kushirikiana na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya limejipanga vizuri kuhakikisha linakomesha vitendo vya uhalifu katika wilaya ya Karagwe
Katika mkutano huo zimeibuka kero mbalimbali kuhusu umeme, barabara, maji pamoja afya na hawa hapa ni baadhi ya wananchi wakitoa kero zao mbele ya mkuu wa wilaya Karagwe Julius Kalanga Laiser.
Kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya Karagwe Dr.Agness Mwaifuge amewataka wananchi kutumia zaidi vituo vya afya vya serikali kutokana na huduma kuboreshwa zaidi na kuwataka wananchi kutumia bima za afya ili kuwa na uhakika wa Matibabu.
Meneja wa wakala barabara za mjini na vijijini TARURA wilayani Karagwe Mhandisi Kalimbula Malimi amesema kuwa serikali iko mbioni kurekebisha barabara zote zilizoathiriwa na mvua.
Naye meneja wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira RUWASA wilayani Karagwe Mhandisi Kasian Wittike amesema serikali itaboresha mtandao wa maji katika mji wa Nyaishozi ili kukidhi mahitaji katika mji huo.