Bashungwa akunwa na uwekezaji wa KARADEA
19 April 2024, 2:39 pm
Elimu ni urithi pekee usio hamishika kwa mwanadamu, tuwapeleke watoto shule ili wapate maarifa.
Na Devid Geofrey:
Waziri wa Ujenzi na mbunge wa jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa viongozi na wasimamizi wa shule za serikali na binafsi kutoa elimu kuhusu matukio ya dharura yanayoweza kutokea katika mazingira ya shule ikiwa ni pamoja na elimu juu ya majanga ya moto ambayo yamekuwa yakitokea.
Bashungwa ameeleza hayo 19 April 2024 baada ya kuzindua bweni jipya la wavulana katika shule ya msingi ya kiingereza KARADEA iliyopo katika kata ya Bugene wilayani Karagwe.
“Ujenzi wa Bweni umezingatia masuala ya dharura pia niwaombe hata kama dharura haipo tutengeneze mazingira ambayo yatawawezesha wanafunzi kupata elimu kuhusu matukio hayo”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amelipongeza shirika la KARADEA kwa kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika shule hiyo na ameahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ambazo zimeendelea kuwa na mchango mkubwa kwa jamii ya watanzania.
Bashungwa amechangia mabati 100 ambayo yatawezesha ujenzi wa madarasa katika shule hiyo ili kuboresha mazingira ya wanafunzi kujifunza na kufundishwa.
Kwa upande wake Lenadius Lemingthon ambaye ni mwalimu mkuu wa shule hiyo amesema bweni lililozinduliwa lina uwezo wa kulaza wanafunzi 320 na lina mahitaji yote muhimu kwa wanafunzi ikiwemo vyoo,bafu,maeneo ya kufulia pamoja na vifaa vinavyotumika wakati wa dharura.