DC Kyerwa aitaka KDCU kuhamasisha matumizi ya miche bora ya kahawa iliyofanyiwa utafiti
6 April 2024, 3:47 pm
Mkuu wa wilaya ya Kyerwa Zaituni Abdallah Msofe akihutubia katika mkutano mkuu wa chama kikuu cha ushirika cha wilaya za Karagwe na Kyerwa, kushoto (aliyekaa) ni Mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Kalanga Laiser. Picha na: Eliud Henry
Uchumi wa wilaya za Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera hutegemea zaidi Kahawa ambayo hutegemea zaidi ubora wake kuanzia mbegu iliyozalishwa hadi uvunaji na kukaushwa kwake.
Na: Eliud Henry
Wananchi wa wilaya za Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera wametakiwa kuendelea kulima zao la Kahawa kwa kutumia mbegu na miche bora iliyozalishwa kitaalamu ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuinua uchumi katika wilaya hizo.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa 37 wa chama kikuu cha ushirika cha wilaya za Karagwe na Kyerwa KDCU LTD Aprili 5, 2024 katika ukumbi wa Rweru Plaza wilayani Kyerwa, mkuu wa wilaya hiyo Zaituni Abdallah Msofe aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo amesema KDCU LTD kwa kushirikiana na wadau wengine wa Kahawa waendelee kusimamia zao likiwa bado lipo mashambani ili kuongeza tija katika zao hilo.
Hata hivyo DC Msofe ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapambania wananchi hasa wakulima wa Kahawa.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Kalanga Laiser amewataka viongozi wa vyama vya msingi vya Ushirika hasa makarani kuwa waaminifu na kuhakikisha wanapokea Kahawa inayokidhi viwango ili iweze kuwanufaisha wakulima
Mkutano mkuu wa 37 wa KDCU Limited umehitimishwa kwa kufanya uchaguzi wa wajumbe wa Bodi mpya ya chama hicho ambapo Mwenyekiti wa bodi aliyechaguliwa ni bw. Fackson Josiah na makamu wake ni Elimeleck Furaha pamoja na wajumbe wengine watakaoongoza chama hicho kuanzia mwaka huu wa 2024.