Wakulima Kagera watakiwa kupanda miti ya matunda kwa wingi
8 November 2023, 8:10 pm
Na Jovinus Ezekiel
Serikali mkoani Kagera imepongeza jitihada zinazoendelea kutekelezwa na taasisi ya KADERES inayohudumia wakulima katika wilaya mbalimbali za mkoa huo kwa kuanzisha mafunzo ya kilimo na uzalishaji wa miche ya miti rafiki kwa mazingira kwa ajili ya kuendeleza kilimo mseto.
Akizungumuza katika hafla ya uzinduzi wa kituo cha mafunzo ya kilimo na uzalishaji wa miche ya miti rafiki kwa mazingira ambayo imefanyika Novemba 7, 2023 katika kijiji cha Kyakakera kata ya Kilimilile wilayani Missenyi, mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatuma Mwasa amesema kuwa serikali ya mkoa wa Kagera imeridhishwa na jitihada zinazoendelea kutekelezwa na taasisi ya KADERES yenye makao yake makuu wilayani Karagwe kwa kuanzisha mafunzo ya kilimo na uzalishaji wa miche rafiki kwa mazingira.
“Jitihada hizi ni nzuri katika kuwainua wakulima wa wilaya ya Missenyi na mkoa wa Kagera ambao watanufaika na fursa hii kwani lengo la KADERES ni kuhakikisha wakulima wanaendeleza kilimo mseto” Amesema Hajat Mwasa.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Missenyi Projestus Tegamaisho amesema kuwa tangu halmashauri ya wilaya hiyo impokee mkurugenzi wa taasisi ya KADERES Bw, Leonard Kachebonaho kuwekeza katika wilaya ya Missenyi serikali ya wilaya Misssenyi inategemea wakulima watanufaika kupitia sekta ya kilimo hasa kupitia mradi wa Biashara ya hewa ukaa.
Naye mkurugenzi wa taasisi ya Kaderes Bw, Leonard Kachebonaho amesema kuwa malengo ya taasisi hiyo kufikia 2040-2050 ni kuhakikisha mkulima wa mkoa wa kagera ananufaika na kilimo chenye tija na kupata soko zuri la mazao anayozalisha mwenyewe ili anufaike kiuchumi.
Hata hivyo miongoni mwa viongozi wa dini akiwemo Askofu Msaidizi wa jimbo katoliki la Bukoba Methodius Kilain na Askofu Dkt Abedinego Kesho mshahara wa kanisa la kiinjili la kilutheli Tanzania dayosisi ya kasikazini magharibi wamesema kuwa dhima ya mradi huu ni nzuri kwani suala la wakulima kupanda miche ya miti rafiki kwa mazingira hasa ya matunda linaweza kuchangia kuinua uchumi wa mkulima katika mkoa wa kagera.