Askofu atabaruku altare parokia ya Businde
18 September 2023, 2:19 pm
Na: Eliud Henry
Askofu wa Jimbo Katoliki Kayanga, Mhashamu Almachius Rweyongeza ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 163 wa Parokia ya Mtakatifu John Chrysostorm-Businde pamoja na kutabaruku altare ya parokia hiyo kwa kuzika masalia ya Mt.Yohane Paulo II kama ishara ya kutoka katika matumizi ya kawaida kwenda kwenye matumizi ya altare.
Maadhimisho hayo yamefanyika Septemba 17, 2023 katika parokiani Businde, ambapo pamoja na mambo mengine, Mhashamu Rweyongeza, amezindua jengo la parokia hiyo pamoja na kubariki vifaa kadhaa vya altare na kubariki jozi 5 za ndoa.
Akitoa homilia mbele ya waumini wa parokia hiyo amesisitiza juu ya faida za kusamehe akisema kukosea ni jambo la kibinadamu ila kusamehe ni jambo la ki-Mungu na kuongeza kuwa kusamehe ni kutakasa kumbukumbu.
Amewaasa waamini kuacha chuki, hasira, ubaya na wivu na kuwa wasiweke mipaka katika kusamehe.
Ameongeza kuwa, msamaha na huruma huleta amani hivyo waamini wamuige Mungu kupitia kwa mwanae Yesu Kristu aliyetamka maneno ya msamaha msalabani.
Katika tukio jingine, Mhashamu Rweyongeza, amekabidhi cheti cha shukrani kutoka Radio Maria Tanzania, kwa wana parokia ya Businde iliyoshika nafasi ya kwanza katika kampeni ya marathon 2023.