Karagwe FM

Padre atoa msaada kwa watoto wenye uhitaji

4 September 2023, 1:02 pm

Mkurugenzi wa idara ya mashirika ya kipapa ya kimisionari Padre David Livingston (wa tatu kutoka kulia) akitoa Msaada wa vyakula,nguo na vifaa vya kujifunzia katika shule ya msingi Mwoleka mseto, Picha na Ospicia Didace

Na Ospicia Didace

Karagwe

Mkurugenzi wa idara ya mashirika ya kipapa ya kimisionari ametoa msaada wa vyakula, nguo na vifaa vya kujifunzia vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tatu kwa wanafunzi wa shule msingi Mwoleka Mseto iliyoko Chabalisa katika kata Nyabiyonza wilayani Karagwe mkoani Kagera.

Baadhi ya wazazi wanawatelekeza watoto wao wenye mahitaji maalumu baada ya kuwafikisha katika shule ya msingi Mwoleka Mseto na kupoteza mawasiliano jambo linalosababisha wafanyakazi wa shule hiyo kuwajibika kuwahudumia kwa kila kitu

Akitoa msaada huo mkurugenzi wa idara ya mashirika ya kipapa ya Kimisionari jimbo Katholiki la Kayanga Padre David Livingston ambaye pia ni Baba Paroko wa Parokia ya Mabira amesema kuwa shirika hilo linalenga kuwapa furaha watoto wote ulimwenguni kwa kuhimiza upendo dhidi yao.

Padre Livingston amesema kuwa msaada huo umetoka kwa waumini kwa lengo la kuleta furaha kwa watoto na kueleza kuwa vitu vilivyoletwa vyenye thamani ya shilingi 3,420,000/= ni pamoja na mchele,sabuni,unga,nguo, daftari na Kalamu.

Naye Mwl mkuu msaidizi wa shule hiyo sister Fransisca Jeremiah ameshukuru idara hiyo kwa kuwapatia msaada huo akisema utasaidia katika malezi ya watoto kitaaluma, kiakili na kiroho kwani watoto hao wana mahitaji mengi ikiwemo mahitaji ya kujifunzia na kufundishia kwa watoto wenye mahitaji maalum.

Pamoja na hayo Sister Fransisca ameeleza kusikitishwa na baadhi ya wazazi wanaowatelekeza watoto wao wenye mahitaji maalum baada ya kuwafikisha shuleni hapo akisema kuwa hupoteza hata masasiliano na kuwajibika kuwahudumia kwa kila kitu.