DC Karagwe: Jamii ielimishwe zaidi juu ya dhana ya uwepo wa meno ya plastiki
12 July 2023, 11:41 pm
Mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Kalanga Laizer ameiomba wizara ya Afya kuendelea kutoa elimu sahihi kwenye jamii juu ya Imani potofu ya uwepo wa Meno ya Plastiki kuwa ni ukatili kwa watoto.
Na Ospicia Didace
Mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Kalanga Laizer ametoa ombi hilo katika ufunguzi wa utoaji elimu sahihi juu ya dhana potofu ya uwepo wa meno ya plastiki inayoendeshwa na shirika la Bridge to Aid Tanzania kwa kushirikiana na wizara ya Afya katika ukumbi wa Angaza mjini Kayanga wilayani Karagwe.
Laizer amesema kuwa elimu ikitolewa na kueleweka vizuri itasaidia kuondokana na imani hizo potofu ambapo ameiomba wizara ya Afya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kutoa elimu zaidi ya dhana potofu iliyojengeka juu ya meno ya plastiki kuanzia kipindi cha ujauzito na mama mjamzito akielewa hata baada ya kupata mtoto hatadanganyika.
Alisema kuwa ni mweli jamii ishaamini katika uwepo wa meno hayo ila taratibu itabadilika akisema kuwa kumtoa mtoto jino bila ganzi tena kwa sipoko ni ukatili kama ulivyo ukatili mwingine.
Udanganyifu unaofanywa na wakunga na watu wanaowang’oa na kusugua meno yanayodhaniwa kuwa ya plastiki ni Hatari kwa watoto na wazazi waonapo dalili kama vile Homa,kutapika na kuharisha wapeleke watoto wao katika vituo vya kutolea huduma kwani wapo wataalam wabobezi na sio kwa kuwapeleka kwa wakunga.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa Bridge to Aid Dr. Nila Jackson amesema kuwa lengo la elimu hiyo ni kuondokana na dhana potofu juu ya meno ya plastiki akieleza madhara yatokanayo na kuwang’oa hayo meno watoto wadogo kuwa ni pamoja na kifo,maumivu makali, kupata magonjwa ya kudumu kama HIV na Homa ya Ini na madhara ya muda mrefu ni pamoja na kutoota meno sambamba na mpangilio mbaya wa meno.
Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi kinywa na meno wizara ya Afya Dr. Baraka Nzobo amekemea vikali udanganyifu unaofanywa na wakunga na watu wanaowangoa na kusugua meno yanayodhaniwa kuwa ya plastiki kuwa wazazi waonapo dalili kama vile Homa,kutapika na kuharisha wapeleke watoto wao katika vituo vya kutolea huduma kwani wapo wataalam wabobezi na sio kwa kuwapeleka kwa wakunga.
Dr. Nzobo ameiomba kamati ya ulinzi na usalama wilayani Karagwe kusaidia kwa ukaribu sana ili kuhakikisha jambo hilo la ukatili kwa watoto linatokomezwa kwa haraka.