Karagwe: Wanaodaiwa kununua ardhi kinyemela watakiwa kuwasilisha nyaraka kwa DC
3 July 2023, 12:44 pm
Serikali wilayani Karagwe imetoa siku saba kwa wananchi walionunua ardhi ya kijiji cha Kahanga kata ya Nyakasimbi wilayani humo kinyume cha sheria kuwasilisha vielelezo vitakavyowezesha kubaini wahusika waliowauzia ardhi hiyo.
Na Eliud Henry
Wakizungumuza katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na mkuu wa wilaya Karagwe Julius Laizer kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi, baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kahanga kata ya Nyakasimbi wilayani Karagwe wamesema kuwa katika kijiji hicho yapo maeneo ambayo yameuzwa na viongozi wa serikali ya kijiji hicho kinyume cha sheria bila kuwashirikisha wananchi.
Miongoni mwa wananchi hao Josia Katabazi na Binemungu Nestory wamesema kwa kuwa maeneo hayo yameuzwa wananchi kwa sasa hawana maeneo ya kulima na kumtaka mkuu wa wilaya kuwachukulia hatua wananchi ambao waliuziwa ardhi hiyo kinyume cha sheria na waliohusika kuwauzia.
Aidha baada ya malalamiko hayo mkuu wa wilaya Karagwe Julius Laizer ametoa siku saba kwa wananchi wanaotuhumiwa kununua ardhi ya kijiji hicho kuwasilisha vielelezo vyao ndani ya siku saba hali itakayowezesha kubaini wananchi waliohusika kuuza ardhi ya kijiji cha Kahanga na kuwataka viongozi wa kijiji hicho kutoa ushirikiano katika suala hilo.
Hata hivyo Bw. Laizer pia ameagiza uongozi wa kijiji hicho kuhakikisha unatatua kero ya mwananchi wa kijji hicho aliyedai kunyang’aywa ardhi baada ya wazazi wake kufariki dunia ili aweze kurudishiwa ardhi yake.