Zenj FM

Masharti magumu kikwazo wenye ulemavu kupata mikopo Zanzibar

13 October 2024, 5:08 pm

Baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao cha kuwasilisha ripoti ya ufuatiliaji wa asilimia 2 ya fedha inayotolewa na serikali kwa ajili ya watu wenye ulemavu,

Na Mary Julius.

Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Asia Abdulsalam Hussein, amesema fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuwafikia watu wenye ulemavu bado hazijawafikia walengwa.

Akizungumza katika kikao cha kuwasilisha ripoti ya ufuatiliaji wa asilimia 2 ya fedha inayotolewa na serikali kwa ajili ya kuwafikia watu wenye ulemavu, utafiti uliolenga kuangalia ni kiasi gani kilitengwa na kiasi gani kimetumikia,  kikao  kilichofanyika katika ukumbi wa UWZ Kikwajuni Unguja, Bi. Asia amesema fedha hizo haziwafikii walengwa kutokana na mikopo hiyo inayolewa kwa vikundi na kuwaunganisha watu wenye ulemavu ni tatizo kwa sababu kila mmoja ana aina yake ya ulemavu na mahitaji yake.

Aidha Mkurugenzi Asia amesema masharti yaliyowekwa yamekuwa magumu na kuwafanya watu wenye ulemavu kushindwa kukidhi vigezo na masharti ya kupatiwa fedha hizo.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Asia Abdulsalam Hussein,

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Michezo kwa Ajili Watu Wenye Ulemavu wa Akili SOZI Omary Bakari Shomari amesema ufuatiliaji walio ufanya umeonyesha kuwa masharti  ya kupatikana kwa fedha hizo ndio kikwazo kikubwa kwa watu wenye ulemavu kufikiwa.

Sauti ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Michezo kwa Ajili Watu Wenye Ulemavu wa Akili SOZI Omary Bakari Shomari

Nao wajumbe waliohudhuria kikao hicho wamewaomba watu wenye ulemavu kujitokeza ili kuomba fedha hizo ambazo ni haki yao na kuiomba serikali kupunguza masharti ya mikopo hiyo kwa watu wenye ulemavu.

Aidha amesema elimu inahitajika ili kuweza kuwashawishi watu wenye ulemavu kujitokeza katika michakato mbalimbali ya kimaendeleo.

Sauti ya wajumbe.

Utafiti huo umedhaminiwa na Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA)