Zenj FM
Zenj FM
01/04/2026, 18:11

Kamati ya Baraza la Wawakilishi imesisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa masheha ili kupunguza matumizi ya dawa za kulevya na pombe haramu. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Machano Othman Said, amesema viongozi hao wana jukumu la kulinda maadili na usalama wa jamii.
Na Mwandishi wetu.
Kamati ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali imesema uwajibikaji na utekelezaji madhubuti wa majukumu ya viongozi wa shehia utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza athari za dawa za kulevya na pombe haramu nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Machano Othman Said, wakati wa kikao cha pamoja na viongozi na watendaji wa Mkoa wa Kusini Unguja, kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Tunguu.
Amesema masheha wana wajibu mkubwa wa kusimamia maadili ya jamii na kudhibiti vitendo vinavyohatarisha usalama, ikiwemo matumizi na biashara ya dawa za kulevya,wizi wa mazao , pamoja na pombe haramu .
Kutokana na hali hiyo, kamati imeitaka serikali kuhakikisha masheha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mikataba yao ya kazi, sambamba na kuimarisha ushirikiano kati yao, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.
Kwa upande wa wajumbe wa kamati hiyo Zaina Abdalla Salum na Mahfoudhi Abdallah Muhamed wamesema kuwepo kwa mikakati madhubuti katika masuala ya udhalilishaji ,migogoro ya ardhi na elimu kutapelekea mkoa huo kuzidi kupiga hatua kimaendeleo hivyo ni vyema kwa viongozi kusimamia vyema majukumu hayo.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mohammed Ali Abdallah, amesema hali ya usalama imeendelea kuimarika, huku akibainisha kuwa matumizi ya mifumo ya mawasiliano ya kielektroniki yameongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya serikali