Zenj FM
Zenj FM
23/03/2026, 16:11

Zaidi ya vijana 250 wa Jimbo Katoliki la Zanzibar wametembelea Hospitali ya Wilaya ya Mbuzini kutoa msaada na faraja kwa wagonjwa ikiwa ni sehemu ya mfungo wa kwaresima.
Na Mary Julius.
Katika kipindi cha mfungo wa kwaresima, vijana zaidi ya 250 wa Jimbo Katoliki la Zanzibar wameonesha moyo wa upendo na huruma kwa kuwatembelea wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbuzini, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza matendo ya huruma na mshikamano wa kijamii.
Akizungumza na Zenj FM, Katibu Msaidizi wa Vijana wa Jimbo hilo, Joseph Cosmas, amesema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kuhamasisha na kudumisha utamaduni wa kufanya matendo ya huruma hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima, ambacho kinahimiza upendo, kujitoa na kusaidiana miongoni mwa waumini.
Ameeleza kuwa vijana hao wamechagua kuitembelea hospitali hiyo ili kuwafikia watu wenye mahitaji maalum, kuwafariji wagonjwa pamoja na kutoa msaada wa hali na mali kulingana na uwezo wao.
Aidha, ametoa wito kwa vyama vingine vya kitume na jamii kwa ujumla kujenga utamaduni wa kuwasaidia wenye uhitaji kila siku, akisisitiza kuwa msaada haupaswi kuwa wa msimu pekee bali endelevu.
Kwa upande wake, Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Mbuzini amewapongeza vijana hao kwa hatua yao ya kujali na kuthamini maisha ya watu wenye mahitaji.
Amesema kuwa vitendo hivyo vina mchango mkubwa katika kuwapa nguvu wagonjwa kisaikolojia na kuleta matumaini mapya katika kipindi chao cha matibabu.
Msaada ulio tolewa ni pamoja na mchele,sukari mafuta ya kupikia sabuni za kuogea sabuni za kufulia dawa ya mswaki miswaki.