Zenj FM

NIC yapendekezwa kuanzisha bima ya takaful

19/03/2026, 22:05

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Balozi Zena Ahmed Said.

Balozi Zena Ahmed Said ameliomba Shirika la Bima la Taifa (NIC) kuangalia uwezekano wa kuanzisha bima ya Takaful, ili kuwasaidia wananchi ambao wana vikwazo vya kiimani kujiunga na huduma za bima.

Na Mary Julius.

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Balozi Zena Ahmed Said, ameliomba Shirika la Bima la Taifa (NIC) kuchunguza uwezekano wa kuanzisha huduma ya bima ya Takaful, ili kuondoa vikwazo vya kiimani vinavyoweza kuwazuia baadhi ya wananchi kunufaika na huduma za bima.

Akizungumza katika futari ya pamoja iliyoandaliwa na NIC na kufanyika katika Golden Tulip Zanzibar Airport Hotel, Balozi Zena amesema sekta ya bima ina fursa kubwa ya kukua.

Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa bima ya Takaful kutasaidia kupanua wigo wa huduma na kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Amesema bima ya Takaful ni mfumo unaokubalika kwa watu wa imani mbalimbali, hivyo inaweza kuwa chachu ya kuongeza ushiriki wa wananchi katika huduma za bima nchini.

Aidha, amelipongeza Shirika la Bima la Taifa kwa kuandaa futari hiyo, akisisitiza kuwa mwezi mtukufu wa Ramadhani ni wakati wa kujikumbusha kumcha Mwenyezi Mungu, kushirikiana, kuwa na moyo wa ukarimu, na kufanya kazi kwa uadilifu huku tukilinda amani ya nchi.

Sauti ya Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Balozi Zena Ahmed Said.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Kaimu Abdi Mkeyenge Mkurugenzi wa maendeleo ya biashara NIC Waziri Kindamba amesema lengo la futari hiyo ni kuwakutanisha wafanyakazi na wadau mbalimbali ili kuimarisha mshikamano na kutafuta baraka katika mwezi wa Ramadhani.

Ameeleza kuwa hafla hiyo imelenga kuwapa motisha waliofunga na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi na wateja, hatua itakayosaidia shirika kuendelea kukua na kupata mafanikio zaidi.

Sauti ya Mkurugenzi wa maendeleo ya biashara NIC Waziri Kindamba.

Katika hafla hiyo, viongozi mbalimbali wa serikali, wakiwemo makatibu wakuu, wamehudhuria ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hiyo  na watendaji wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.