Zenj FM
Zenj FM
06/03/2026, 14:30

Na Mary Julius.
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Juma Malik Akil, amesema sekta ya fedha nchini inaendelea kukua kwa kasi siku hadi siku kutokana na mchango wa wadau mbalimbali, wakiwemo taasisi za kifedha kama KCB Bank ambazo zimekuwa mstari wa mbele kupanua huduma za kifedha na kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Akizungumza wakati wa futari iliyoandaliwa na KCB Sahl Banking kwa wateja wake, iliyofanyika katika Golden Tulip Zanzibar Airport, Waziri huyo aliipongeza benki hiyo kwa juhudi zake za kupanua wigo wa huduma za kibenki, hususan huduma za kifedha zinazozingatia misingi ya Shariah kupitia Sahl Banking.
Dk. Akili amesema Serikali inatambua mchango wa KCB katika kukuza uchumi na kuendeleza sekta ya fedha, huku akisisitiza kuwa milango iko wazi kwa taasisi hiyo kushirikiana na Serikali katika kutekeleza ajenda ya maendeleo, ikiwemo uwekezaji katika miradi ya miundombinu na utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shariah ya KCB, Sheikh Khamis Mataka, amesema kupitia kitengo cha Sahl Banking benki hiyo imelenga kutoa huduma mbalimbali za kifedha zinazozingatia misingi ya sheria za Kiislamu.
Amesema tukio la futari hiyo limeonyesha kiwango kikubwa cha imani ambacho wateja wanacho kwa benki hiyo, huku akibainisha kuwa mwezi wa Ramadhani unawakumbusha wafanyabiashara umuhimu wa kufanya biashara kwa uaminifu, uwazi na kumcha Mungu.
Naye Meneja Mkuu wa Kitengo cha KCB Sahl Banking, Amour Muro, amesema lengo la futari hiyo ni kuimarisha uhusiano na wateja wa benki hiyo na kurudisha shukrani kwa imani wanayoendelea kuionesha.
Amesema KCB imeaona umuhimu wa kuiunga mkono Serikali katika juhudi za kukuza uchumi na kuwa sehemu ya maendeleo ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo.
Aidha,amesema benki hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kijamii kwa kushirikiana na jamii katika kukuza maendeleo ya kiuchumi, huku ikijivunia kupanua huduma zake kupitia tawi jipya la Mkunazini Zanzibar.