Zenj FM

Zanzibar yaongeza ubora wa afya kupitia Ushirikiano na sekta binafsi

01/03/2026, 17:11

Naibu Waziri wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji Hassan  Khamis Hafidh akizungumza katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Saifee Hospital Zanzibar Limited, iliyofanyika katika Hotel Madinat Al Bahr.

Na Mary Julius.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na za kisasa za afya.

Kauli hiyo imetolewa kwa niaba ya Waziri wa Afya Zanzibar, Saada Mkuya Salum, katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Saifee Hospital Zanzibar Limited, iliyofanyika katika Hotel Madinat Al Bahr.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji Hassan  Khamis Hafidh  amesema kuwa hapo awali baadhi ya wananchi hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu dhana ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

Amesema kwa sasa matokeo ya ushirikiano huo yanaonekana wazi kupitia kuimarika kwa huduma zinazotolewa katika hospitali za wilaya zinazosimamiwa na Saifee Hospital Zanzibar Limited.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuona matunda ya ushirikiano huo, ikiwemo kuongezeka kwa ubora wa huduma, upatikanaji wa wataalamu pamoja na kuimarika kwa miundombinu ya afya.

Aidha, ameishukuru Saifee Hospital Zaznibar kwa kuandaa futari hiyo iliyowakutanisha viongozi wa Wizara ya Afya, wadau wa sekta ya afya pamoja na wafanyakazi wa hospitali hiyo, akibainisha kuwa mikutano ya aina hiyo huimarisha mashirikiano na kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.

Sauti ya Naibu Waziri wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji Hassan Khamis Hafidh.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Saifee Hospital Zanzibar Limited Dr Murtaza Haiderbhai  amesema kupitia ushirikiano huo na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Wizara ya Afya, hospitali hiyo imefanikiwa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 1,000, hatua inayochangia kupunguza tatizo la ajira na kuimarisha utoaji wa huduma za afya. Amesisitiza kuwa afya na ajira ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii.

Ameongeza kuwa kupitia usimamizi wa hospitali 10 za wilaya, wameimarisha upatikanaji wa dawa muhimu, kuboresha huduma za maabara, kuimarisha huduma za mama na mtoto pamoja na kuendeleza mifumo ya kidijitali inayorahisisha utoaji wa huduma.

Aidha Mkurugenzi Mkuu amesema saifee imefanikiwa kuwaleta madaktari bingwa wa fani mbalimbali waliotekeleza kambi maalum za matibabu, hatua iliyopunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa.

Sauti ya Mkurugenzi Mkuu wa Saifee Hospital Zanzibar Limited Dr Murtaza Haiderbhai.