Zenj FM
Zenj FM
25 February 2026, 4:05 pm

Na Berema Suleiman.
Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar imesema jumla ya mienendo ya vyombo vya baharini kwa mwezi wa Januari 2026 imefikia 1,211, ikiwa ni upungufu wa asilimia 35.6 ikilinganishwa na mienendo 1,879 iliyorekodiwa mwezi Januari 2025.
Akiwasilisha takwimu hizo, Mtakwimu Raya Mohammed Mahfoudh kutoka Kitengo cha Usafiri na Mawasiliano amesema katika mwezi wa Januari 2026, jumla ya mienendo ya meli za kigeni ilikuwa 6, huku meli za ndani zikiwa 654 na majahazi 551.
Kwa upande wa usafiri wa abiria kwa njia ya baharini, jumla ya abiria 371,942 waliingia na kutoka katika bandari za Zanzibar mwezi Januari 2026, sawa na ongezeko la asilimia 31.7 ikilinganishwa na abiria 282,490 waliorekodiwa mwezi Januari 2025.
Aidha, mienendo 7,152 ya ndege imerekodiwa mwezi Januari 2026, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.6 ikilinganishwa na mienendo 6,586 ya ndege iliyorekodiwa mwezi Januari 2025.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (B.O.T) upande wa Zanzibar, Hamad Khamis, amesema uanzishwaji wa utolewaji wa takwimu za usafirishaji utasaidia kuimarisha ufuatiliaji wa uchumi kupitia sekta ya usafirishaji pamoja na kufungua fursa zaidi za uwekezaji.
Naye Mchumi Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dk. Stella Ngoma Hassan, amesema usafiri wa ndege ni miongoni mwa nguzo muhimu zinazochochea ukuaji wa uchumi wa taifa, hususan kupitia sekta ya utalii.