Zenj FM

Hakuna msamaha kwa madereva wakiukaji wa sheria Zanzibar

10 February 2026, 2:37 pm

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Badria Antai,akizungumza na waandishi wa habari katika kikao cha pili cha kutoa taarifa ya wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zaznibar.

Na Mary Julius.

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar imewasisitiza madereva wote kuzingatia sheria za usafiri na usalama barabarani ili kulinda maisha ya wananchi wa Zanzibar.

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Badria Antai, amesema hatua zinazochukuliwa na serikali zimeanza kuleta matokeo chanya, ambapo makosa ya barabarani yamepungua kutoka makosa 1,190 mwezi Desemba  mwaka 2025 hadi 1,015 mwezi Januari 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, Naibu Waziri amesema licha ya mafanikio hayo, bado kuna changamoto ya baadhi ya madereva kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo wa kasi pamoja na kuendesha bila kuwa na leseni halali.

Amesisitiza kuwa wizara haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya dereva yeyote atakayekamatwa akikiuka sheria hizo.

Sauti ya Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Badria Antai,

Aidha, Naibu Waziri amewataka waendesha bodaboda kuzingatia masharti ya upakiaji wa watoto, akisisitiza kuwa mtoto mwenye umri chini ya miaka saba anapaswa kusafirishwa akiwa na mtu mzima.

Pia wizara imetoa onyo kali kwa waendesha boda boda wanaopakia watoto wengi katika chombo kimoja, hali ambayo inahatarisha maisha na usalama wa watoto hao.

Naibu Waziri amesisitiza kuwa yeyote atakayebainika kubeba watoto wengi kinyume na sheria, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Sauti ya Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Badria Antai.