Zenj FM
Zenj FM
4 February 2026, 11:12 pm

Na Mary Julius.
Makamo Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, Ismail Jussa, ameiomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kusitisha zoezi la kuteketeza nyaraka na vifaa vya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 hadi mashauri yote yaliyopo mahakamani yatakapomalizika.
Makamo Mwenyekiti huyo ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho,vuga Zanzibar.
Amesema nyaraka hizo bado ni muhimu na zinahitajika kama vielelezo katika mashauri yanayoendelea mahakamani, hivyo kuteketezwa kwake kunaweza kuathiri mwenendo wa haki.
Jussa amesema tangu tarehe 21 Januari, 2026, chama hicho kimekuwa na maombi ya kisheria mahakamani yakiomba nyaraka muhimu za uchaguzi zikabidhiwe kwa ajili ya matumizi ya ushahidi, lakini ZEC imeshindwa kutekeleza wajibu huo hadi sasa.
Aidha, Ismail Jussa ametoa wito kwa mamlaka zote zinazohusika kuhakikisha kuwa nyaraka na vifaa vyote vya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 vinahifadhiwa chini ya ulinzi madhubuti hadi taratibu zote za kisheria zitakapokamilika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jaji George Joseph Kazi, akijibu hoja zilizo tolewa na chama cha act wazalendo amesema zoezi la kuteketeza nyaraka za Uchaguzi Mkuu linafanyika kwa mujibu wa sheria.
Ameeleza kuwa kifungu cha 98(3) cha Sheria ya Uchaguzi Namba 4 ya mwaka 2018 kinaruhusu nyaraka za uchaguzi kutunzwa kwa muda wa siku 90 kabla ya kuteketezwa.
Jaji Kazi ameongeza kuwa kama chama hicho kilikuwa na haja ya kuzuia kuteketezwa kwa nyaraka hizo, kingeweza kuwasilisha pingamizi mahakamani.
Amesema kutokana na kutokuwepo kwa zuio lolote la mahakama, Tume ya Uchaguzi inaendelea na zoezi hilo kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.