Zenj FM
Zenj FM
3 February 2026, 10:03 pm

Na Mary Julius.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 13 wanaohusishwa na wizi wa vifaa vya ujenzi kwa njia ya udanganyifu, unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na utapeli wa fedha, kufuatia operesheni iliyoanza tarehe 31 Januari 2026.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Thadei Mchomvu, ameyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika ofisi yake Madema.
Akizungumza kuhusu hali ya usalama barabarani, Kamanda Mchomvu amesema kumekuwepo na ongezeko la ajali zinazosababishwa na uzembe wa baadhi ya madereva, hususan kutofuata sheria za usalama barabarani, hali inayosababisha vifo na ulemavu kwa wananchi.
Amesema ili kudhibiti ajali hizo, Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limeanzisha Doria Maalum za Barabara Kuu (Highway Patrol) zitakazofanyika mara kwa mara, huku akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya dereva yeyote atakayekiuka sheria za usalama barabarani.