Zenj FM
Zenj FM
3 February 2026, 9:02 pm

Na Mary Julius.
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeidhinisha rasmi zoezi la kuteketeza nyaraka zote zilizotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025, baada ya kukamilika kwa muda wa siku 90 tangu kumalizika kwa uchaguzi huo, kwa mujibu wa matakwa ya kisheria.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Tume kilichofanyika tarehe 2 Februari, 2026, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria ya kuhakikisha mchakato mzima wa uchaguzi unakamilika kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.
Katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji George Kazi, amesema zoezi hilo linafanyika kwa kuzingatia kifungu cha 98(3) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018, ambacho kinaitaka Tume kuharibu nyaraka zote zinazohusiana na Uchaguzi Mkuu baada ya kupita siku 90 tangu kukamilika kwa uchaguzi husika.
Amefafanua kuwa kabla ya kuidhinisha utekelezaji wa zoezi hilo, Tume ilijiridhisha kuwa hakuna amri yoyote ya mahakama inayozuia utekelezaji wa hatua hiyo, jambo lililoiwezesha kutekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa sheria baada ya kukamilika kwa muda uliopangwa.
Aidha, Jaji Kazi amewataka wadau wote wa uchaguzi kushirikiana ipasavyo katika utekelezaji wa zoezi hilo ili kuhakikisha linafanyika kwa mafanikio, kwa uwazi na kwa kuzingatia kikamilifu misingi ya kisheria pamoja na taratibu zilizowekwa.