Zenj FM

Kambi ya matibabu bure kuinufaisha Zanzibar

23 January 2026, 5:08 pm

Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya Zanzibar Msafiri Marijani (aliyevaa tai nyeusi) akiwa na Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald ( kati) Dkt. Robert Moshiro, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Delila Kimambo .

Na Mary Julius.

Katika kuhakikisha jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla wanakuwa na afya njema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar na kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania, imeandaa kambi maalum ya siku nne ya uchunguzi na matibabu ya maradhi yasiyoambukiza bure.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Idara ya Tiba Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Msafiri Marijani amesema mkakati wa serikali wa kuandaa kambi hizo ni kusaidia kufanyika kwa uchunguzi wa mapema wa maradhi yasiyoambukiza ili kuyagundua mapema na kuzuia vifo vinavyotokana na maradhi hayo.

Ameeleza kuwa serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kutokana na gharama kubwa za matibabu ya maradhi hayo, hivyo uwepo wa kambi hiyo itakayofanyika kuanzia Februari 3 hadi 6 mwaka 2026 utasaidia kuwatambua wananchi wenye maradhi hayo na kuwapatia matibabu pamoja na ushauri wa kitaalamu.

Amefafanua kuwa kambi hiyo itaongozwa na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na madaktari wa hospitali za Zanzibar, ambapo vipimo mbalimbali vitafanyika pamoja na kutolewa  kwa dawa na ushauri nasaha kwa wagonjwa watakaobainika kuwa na maradhi hayo.

Aidha, ameishukuru Vodacom Tanzania kwa kuiweka Zanzibar katika mkakati wake wa kuboresha afya za jamii.

Sauti ya Mkurugenzi Idara ya Tiba wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Msafiri Marijani.

Kwa upande wake, Dkt. Robert Moshiro, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Delila Kimambo, amesema wamekuwa wakishirikiana na Vodacom Tanzania tangu Julai mwaka jana katika kuendesha kambi za matibabu na uchunguzi wa bure, ambapo takribani wananchi 3,500 wamenufaika na huduma hizo.

Amesema dhamira ya kambi hizo ni kuwafikishia wananchi huduma za afya karibu na maeneo yao, hususan huduma za uchunguzi na matibabu ya maradhi yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, saratani, pamoja na uchunguzi wa magonjwa ya masikio, pua na koo, afya ya uzazi kwa kina mama, macho na meno.

Ameongeza kuwa huduma hizo zitatolewa bure katika Uwanja wa new Amaan Complex, kwa kushirikiana na madaktari wa Muhimbili na Zanzibar kwa lengo la kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu.

Sauti ya Dkt. Robert Moshiro.

Naye Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, Ameeleza kuwa tangu mwaka 2023, Vodacom imekuwa ikitekeleza mkakati wa uwekezaji wa kijamii na hadi sasa imefikia mikoa tisa Tanzania Bara na kunufaisha zaidi ya Watanzania 10,000, huku lengo likiwa kuwafikia watu milioni moja.;

Aidha ameihimiza jamii ya Wazanzibari kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kambi hiyo, kwani huduma zote zitatolewa bure, na kutoa fursa adimu ya kuonana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Sauti ya Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald.