Zenj FM

Chuo cha uhamiaji Kitogani kuongeza ufanisi kwa maafisa

9 January 2026, 12:28 am

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiweka jiwe la msingi la jengo la Chuo cha Mafunzo cha Idara ya Uhamiaji Zanzibar kilichopo Kitogani, Mkoa wa Kusini Unguja.

Na Ivan Mapunda.

Kuanzishwa kwa chuo cha mafunzo cha Idara ya Uhamiaji Zanzibar ni hatua muhimu katika kuwaongezea uwezo wa kitaalamu, kiutendaji na kimaadili maafisa na askari wa Idara ya Uhamiaji Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi la chuo cha Mafunzo ya Idara ya Uhamiaji Kitogani, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema kupitia chuo hicho Maafisa wa uhamiaji wataweza kujengewa uwezo katika masuala ya udhibiti wa mipaka, usalama wa taifa, matumizi ya teknolojia, sheria za uhamiaji na kuheshimu haki za binaadamu jambo ambalo litaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kulinda maslahi ya nchi.

Hemed ameuagiza uongozi wa Idara ya uhamiaji kwamba chuo hicho kisiwe kwa ajili ya kutoa mafunzo ya awali pekee bali kitoe mafunzo ya mara kwa mara kwa maafisa, kufanya tafiti, kubadilisha uzoefu na Mataifa mengine duniani ili Idara ya Uhamiaji iendelee kuongeza hadhi zaidi katika masuala ya kiuhamiaji kwa ngazi ya Kikanda na Kiamtaifa.

Sauti ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ali Hassan ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupatiwa boti kwa ajili ya kufanyia doria baharini ambayo itasaidia kudhibiti mipaka ya baharini, kudhibiti wahamiaji haramu pamoja na kufanya doria za visiwani kwa lengo la kuhakikisha usalama na utulivu kwa watalii wanaofika visiwani humo.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa chuo hicho kutaleta mageuzi makubwa Zanzibar kwa kuwa chachu ya kuboresha mashirikiano ya kiutandaji nadani na nje ya nchi.

Sauti ya Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ali Hassan.

Akisoma taarifa ya kitaalamu juu ya ujenzi wa chuo hicho, Katibu Mkuu Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratib na Baraza la Wawakilishi Dkt. Islam Seif Said amesema ujenzi wa jengo hilo umetekelezwa kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria uliogharimu shilingi za Kitanzania zaidi ya Bilioni kumi na mbili ambalo litalaza wanafunzi 320 kwa kila jengo na kwenda kutatua changamoto ya maeneo ya kufanyia mafunzo na kupatikana mazingira mazuri na salama ya kuishi maafsa wanapokuwa mafunzoni.

Sauti ya Katibu Mkuu Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratib na Baraza la Wawakilishi Dkt. Islam Seif Said.