Zenj FM

Polisi Zanzibar kuendelea kuimarisha ushirikiano na wananchi

8 January 2026, 10:18 am

Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo, akizungumza wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Watendaji wa Polisi Jamii kwa ngazi ya Mikoa na Wilaya za Unguja na Pemba yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Polisi Zanzibar.

Na Denis Mtamwega

Jeshi la Polisi nchini limesema litaendelea kuimarisha ushirikiano wake na wananchi kupitia miradi mbalimbali ya Polisi jamii ili kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarika huku wahalifu wakichukuliwa hatua kali za kisheria.

Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo, ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Watendaji wa Polisi Jamii kwa ngazi ya Mikoa na Wilaya za Unguja na Pemba yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Polisi Zanzibar.

Amesema, jukumu la kuimarisha usalama na amani linapaswa kutekelezwa na kila mwananchi, hivyo Jeshi la Polisi litahakikisha linashirikiana na viongozi wengine wa serikali ili kupanga mikakati ya pamoja yenye lengo la kutunza amani kwenye maeneo yao.

Aidha amewataka Polisi shehia ambao ni wawakilishi wa Jeshi la Polisi katika ngazi ya shehia, kufanya kazi kwa kuzingatia nidhamu, weledi na uadilifu na kutenda kwa kuzingatia haki.

Sauti Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo.

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Henry Mwaibambe, amesema ushiriki wa Polisi

Shehia katika kutoa elimu kwa jamii umerahisisha kuimarika kwa hali ya usalama na amani na kuifanya

jamii kutambua viashiria vya uhalifu kwenye maeneo yao na kuviripoti kwenye mamlaka husika.

Mafunzo hayo ya siku moja yanalenga kuwajengea uwezo Watendaji wa Polisi Jamii ambao ndio

kiunganishi kikubwa kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.