Zenj FM
Zenj FM
19 November 2025, 5:41 pm

Na Mary Julius.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha utoaji wa huduma jumuishi kwa watu wenye ulemavu, hususan katika kukuza na kusambaza matumizi ya lugha ya alama kwenye sekta mbalimbali.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wakalimani wa Lugha ya Alama Zanzibar yaliyofanyika Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni, Katibu wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamisi Debe, amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha kila taasisi inayotoa huduma kwa jamii inakuwa na uwezo wa kutumia lugha ya alama.
Amesema tayari sekta ya afya imeanza utekelezaji wa mpango wa kuhakikisha kila kituo cha afya kinakuwa na mkalimani wa lugha ya alama, huku sekta ya elimu ikisonga mbele na mpango wa kuyapatia skuli madarasa maalum ya kufundisha lugha hiyo, sambamba na kuwahamasisha wazazi kujifunza ili kuimarisha mawasiliano na watoto wenye ulemavu.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa SHIJUWAZA, Ali Omar Makame, amesisitiza umuhimu wa kuongeza idadi ya wakalimani wa lugha ya alama nchini.
Makamo mwenyekiti Ametoa mfano wa kipindi cha uchaguzi ambapo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilihitaji wakalimani katika kila kituo, lakini mpango huo haukutekelezeka kutokana na uhaba wa wataalamu hao.
Ameiomba Serikali kuweka silabasi rasmi ya kufundisha lugha ya alama katika skuli na vyuo, pamoja na kuanzisha bodi maalum ya kusimamia mafunzo na viwango vya ukalimani.
Naye Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wakalimani wa Lugha ya Alama Zanzibar (JUWALAZA), Kheri Mohammed Simai, amesema maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika Kaskazini ili kuongeza uelewa katika maeneo ambayo bado yanahitaji mwamko.
Kwa upande wa jamii ya watu wenye ulemavu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Kaskazini Unguja, Haji Khamisi Nyange, amesema mkoa huo umeanza kupata madarasa ya lugha ya alama, lakini bado unahitaji fursa zaidi ili kuongeza idadi ya wataalamu.
Aidha, ameiomba Serikali kuwachukulia hatua wazazi wanaowaficha watoto wenye ulemavu na kuwanyima haki ya kupata elimu.