Zenj FM
Zenj FM
17 November 2025, 4:57 pm

Mkurugenzi wa Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) Ali Machano ameiomba jamii kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali zilizoandaliwa na jumuiya hiyo kuelekea maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani.
Ameeleza kuwa mafunzo maalum yameandaliwa, ambayo yataisaidia jamii kufahamu kwa undani mbinu sahihi za kuishi na kuwatendea haki watu wenye aina mbalimbali za ulemavu.
Akizungumzia uteuzi wa Baraza jipya la Mawaziri, Mkurugenzi huyo amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuunda baraza lenye ushirikishwaji mpana, ikiwemo kuteuliwa kwa mtu mwenye ulemavu katika baraza hilo jambo alilolitaja kuwa ni hatua muhimu katika kujenga usawa na ujumuishi.
Aidha, amemuomba waziri huyo kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu hawasahauliki katika upatikanaji wa fursa mbalimbali zinazowahusu moja kwa moja, ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.