Zenj FM
Zenj FM
6 November 2025, 5:12 pm

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) iliweka mipango bora iliyowezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu kwa amani na bila ya vikwazo vyovyote.
Na Ivan Mapunda.
Mwenyekiti wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Abdulwakili H. Hafidhi, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuhakikisha Uchaguzi Mkuu umefanyika kwa amani, utulivu na uwazi.
Akizungumza na Zenj FM, Mwenyekiti Hafidhi amesema watu wenye ulemavu Zanzibar wamefarijika kwa jinsi uchaguzi ulivyofanyika kwa utulivu na usalama, akieleza kuwa uchaguzi wa mwaka huu umekuwa bora zaidi ikilinganishwa na chaguzi zilizopita, kwani hakukuwa na changamoto zozote kubwa kwa watu wenye ulemavu.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za viongozi wakuu wa nchi wakiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye katika kila hatua amekuwa akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi.

Aidha, Mwenyekiti Hafidhi ameipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kuweka mipango bora iliyowezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu kwa amani na bila ya vikwazo vyovyote.
Pamoja na hayo, Mwenyekiti amewaonya vijana kuacha kutumika vibaya na kuwataka kutafakari kwa kina mambo wanayoambiwa kabla ya kuchukua hatua yoyote.
Aidha amehimiza vijana kutumia akili na busara katika kubainisha mambo yanayowahusu, ili kuendelea kujenga jamii yenye umoja, upendo na amani.