Zenj FM
Zenj FM
5 November 2025, 11:02 pm

Katibu wa Baraza, Raya Issa Mselem, amesema kuwa uchaguzi wa Spika ni shughuli ya kwanza inayofanywa na wajumbe kabla ya kula kiapo cha uaminifu, kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 70 cha Katiba.
Na Mary Julius.
Baraza la 11 la Wawakilishi linatarajiwa kuanza mkutano wake wa kwanza kesho Chukwani, Zanzibar, ambapo miongoni mwa shughuli kubwa ni uchaguzi wa Spika wa Baraza.
Akizungumza na vyombo vya habari, Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Mselem, amesema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 73 (1), wajumbe wateule watachagua Spika kutoka miongoni mwao au mtu mwenye sifa za kuwa Mwakilishi.
Amesema uchaguzi wa Spika ndiyo shughuli pekee anayoifanya Mjumbe kabla ya kula kiapo cha uaminifu, kwa mujibu wa kifungu cha 70 cha Katiba.
Baada ya uchaguzi huo, Katibu wa Baraza atamuapisha Spika mteule, kisha Spika atawaapisha wajumbe wote.
Aidha, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kulizindua rasmi Baraza hilo na kutoa maelekezo yake.
Wakati huohuo, wagombea wa nafasi ya Spika wamejitokeza kuchukua fomu, akiwemo aliyekuwa Spika wa Baraza la 10, Zubeir Ali Maulid kutoka CCM, ambaye amesema ana imani na chama chake na uzoefu wa kuongoza Baraza hilo kwa vipindi viwili vilivyopita.
Wengine waliotangaza nia ni Suleiman Ali Khamis wa ADC, aliyesema ujio wake unatokana na wito wa Rais kuwahamasisha vijana kugombea nafasi za uongozi; Naima Salum Hamad wa UDP, na Chausiku Khatib Mohammed wa NLD.