Zenj FM
Zenj FM
19 October 2025, 9:35 pm

Na Ivan Mapunda
Kwa mara ya kwanza katika historia ya siasa za vyama vingi nchini Tanzania, wagombea Urais wanawake wamejitokeza kwa wingi na kwa nafasi ya juu ya kisiasa kuliko wakati mwingine wowote.
Uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka huu umeweka rekodi mpya kwa namna wanawake walivyojitokeza kuwania nafasi za juu za uongozi.
Historia hii mpya imeandikwa kutokana na ongezeko la wagombea wanawake wanaowania nafasi mbali mbali za uongozi zikiwemo za urais na ugombea mwenza .
Hatua hii inaonyesha mafanikio makubwa ya mapambano ya usawa wa kijinsia ,demokrasia na mustakabali wa taifa.
Wakati katika chaguzi zilizopita wanawake walihesabika kwa vidole, sasa 2025 unakuwa mwaka wa kihistoria ambao uwepo wao unaleta uzito mpya katika mijadala ya kisiasa.
Historia fupi ya wanawake kugombea urais Tanzania
Mara ya kwanza jina la mwanamke lilionekana kwenye karatasi za kura za urais ilikuwa mwaka 2005, alipogombea Anna Senkoro kupitia chama cha PPT maendeleo. Ingawa alishika nafasi ya nane kati ya wagombea kumi, hatua yake ilifungua njia kwa wengine.
Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995 na uliofuata wa 2000 hakukuwa na mgombea urais mwanamke.
Miaka kumi baadaye, Anna Mghwira wa ACT Wazalendo alikuja na kushika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa 2015, hatua iliyoanza kuonyesha uthubutu wa wanawake kwenye nafasi za juu za uongozi wa nchi.
Lakini hata hivyo, katika uchaguzi huo na ule wa 2020, nafasi ya wanawake iliendelea kuwa finyu.
Cecilia Mwanga (Demokrasia MAKINI) na Queen Sendiga (ADC) waligombea mwaka 2020, lakini walimaliza katika nafasi za chini.
Hatua kubwa zaidi ilikuja mwaka 2021, wakati aliyekuwa mgombea mwenza wa Rais John Magufuli katika uchaguzi wa 2015 na 2020, Samia Suluhu Hassan alipoapishwa kuwa Rais kufuatia kifo cha Magufuli.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya tanzania na Afrika Mashariki, nchi iliongozwa na Rais mwanamke. Tukio hilo huenda likawa chachu ya mabadiliko ya siasa za tanzania.
Tangu wakati huo, mjadala kuhusu nafasi ya wanawake kwenye uongozi ukapata msukumo mpya.
Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kati ya wagombea 30 wa nafasi ya Urais na Makamu wa Rais, wanawake walikuwa saba pekee, sawa na asilimia 23.3, kati ya hao watano ndio waliotoka Zanzibar.
Mwaka 2025 ni wa rekodi mpya ya wanawake.
Kwa upande wa urais wapo wanawake 4 wanaosaka kura za kuomba ridhaa ya wananchi .
Wa kwanza ni Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye anaomba nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM.
Samia anaingia kwenye kinyang’anyiro akibeba rekodi ya kuwa kiongozi wa kwanza mwanamke kuongoza Tanzania kabla na baada ya kupata uhuru na sasa anatetea nafasi yake ya uongozi wa juu.
Mwajuma Noty Mirambo wa UMD, mwanasiasa aliyeanzia kwenye michezo na baadaye akajitosa kwenye udiwani kabla ya kugombea ubunge mara kadhaa. Safari yake imekuwa ya kupanda na kushuka, lakini sasa anasema amejiandaa kwa nafasi ya juu kabisa.
Saum Hussein Rashid wa UDP, ambaye kwa sasa ndiye katibu mkuu wa chama hicho, akisisitiza ajenda ya usawa wa kijinsia na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, ni mgombea mwingine aliyeingia kwenye debe.
Sio tu kwa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hata kwa nafasi ya urais wa Zanzibar Laila Rajab Khamis wa chama cha NCCR Mageuzi kwa mara ya kwanza amejitokeza hadharani kwenye jukwaa la siasa za urais akiwakilisha sauti mpya za wanawake kutoka nje ya vyama vikubwa.
Hii ni hatua muhimu ,kwa sababu historia ya siasa nchini imekua ikitawaliwa na majina ya kiume katika kinyang’anyiro cha urais .
Zaidi ya wagombea hao, vyama kumi vimewateua wanawake kama wagombea wenza wa urais.
Hii ni mara ya kwanza tanzania kushuhudia idadi hiyo kubwa ya wanawake kuwania kushika nafasi za juu za uongozi wa nchi.
Wakati wagombea wenza mara nyingi hupatikana kwa vigezo vya kisiasa na kijiografia, mwaka huu uteuzi umeonyesha msisitizo wa wazi wa vyama kuonyesha kujali usawa wa kijinsia.
Kwa ujumla, vyama 18 viko kwenye mbio za urais, na hatua ya vyama vidogo kumteua mwanamke imeongeza hamasa kwamba huu ni uchaguzi wa wa mabadiliko kwa wanawake.
Ingawa wagombea hao huenda wakakabiliwa na changamoto za kukubalika kwa upana, ishara iliyotumwa tayari ni kubwa na inabadilisha historia ya siasa nchini.

Maoni ya wachambuzi wa siasa
Wachambuzi wanasema uamuzi wa vyama kuwasimamisha wanawake unaakisi mabadiliko ya kijamii na kisiasa yaliyopata nguvu zaidi ndani ya miaka 15 iliyopita.
Elimu, uhamasishaji wa haki za wanawake na mfano wa Rais Samia vinatajwa kama sababu kuu zinazoongeza imani kwa wanawake kushika nafasi za juu.
“kuna mwamko fulani wa jamii na ni kweli idadi imeongezeka, lakini ukilinganisha na wagombea wanaume kuna kupwaya”, anasema Ali Makame , mchambuzi wa siasa.
Wakati mwingine, vyama huona ni busara kisiasa kuonyesha sura mpya kupitia wagombea wanawake, hasa katika zama ambazo wapiga kura vijana na wanawake wanachangia sehemu kubwa ya idadi ya wapiga kura.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema kuwa sasa ndio wakati wa viongozi wanawake kuchukua hatua madhubuti na kuleta mabadiliko halisi katika safari zao za uongozi.
“huu ndio wakati umuhimu wa kutumia maarifa waliyonayo kuleta ushawishi na matokeo chanya katika jamii”. Dkt. Jingu amesisitiza
Wakati historia ya Bibi Titi Mohammed, Lucy Lameck na viongozi wengine wa mwanzo inaendelea kukumbukwa, kizazi kipya kinaongeza sura mpya kwenye simulizi ya taifa.
Lakini mwaka huu, nchi inashuhudia ongezeko la wanawake wanaowania urais sambamba na wagombea wenza.
Hali hii ni ishara kwamba, historia ya siasa za Tanzania zinafunguka upya na sura ya mwanamke katika uongozi inaanza kupata nafasi yake.
Tanzania Itafanya Uchaguzi Wake Mkuu Oktoba 29, 2025 Ambapo Wapigakura 37, 655,559 Wamejiandikisha Kupiga Kura Katika Majimbo 272.