Zenj FM
Zenj FM
18 October 2025, 11:38 pm

Na Mary Julius.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Thabiti Idarous Faina, amesema jumla ya shilingi milioni 903,327,300 zimetumika katika uchapaji wa karatasi za kura za Urais wa Zanzibar, Uwakilishi na Udiwani ambazo zitatumika katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza katika hafla ya kupokea karatasi hizo za kura iliyofanyika katika ghala kuu la ofisi za Tume Maisara, Zanzibar, Mkurugenzi Faina amesema bajeti iliyokuwa imetengwa kwa kazi hiyo ilikuwa shilingi bilioni 1.245.592.000, hivyo uchapaji huo umefanyika kwa gharama nafuu bila kuathiri ubora.
Mkurugenzi Ameeleza kuwa kupokelewa kwa karatasi hizo ni hatua muhimu katika kukamilisha maandalizi ya vifaa muhimu vya uchaguzi.
Mkurugenzi Faina amebainisha kuwa karatasi hizo zimechapishwa na Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar hatua iliyowezesha usimamizi wa karibu na kupunguza changamoto za usafirishaji na ucheleweshaji wa vifaa kutoka nje ya nchi.
Aidha Mkurugenzi Faina amesema katika kuwajali watu wenye mahitaji maalum Tume hiyo imeandaa karatasi maalum za kura zenye mwongozo mahsusi kwa watu wasioona.
Amesema karatasi hizo zimetengenezwa kwa mfumo maalum wa usaidizi (braille) ili kutoa fursa kwa wapiga kura wasioona kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura bila kikwazo chochote.
Nao Baadhi ya wawakilishi wa vyama vya siasa waliokuwepo katika hafla hiyo wameipongeza Tume kwa kuendesha mchakato huo kwa uwazi, ushirikiano na weledi, hatua ambayo wamesema itaongeza uaminifu na kupunguza malalamiko kuhusu uchaguzi.