Zenj FM
Zenj FM
15 October 2025, 3:53 pm

Na Mary Julius.
Jeshi la Polisi Kanda ya Zanzibar limeendesha operesheni maalum katika mikoa mitatu ya Unguja kufuatia kuongezeka kwa matukio ya wizi wa pikipiki, ambapo jumla ya watu 17 wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mtandao wa wizi na uuzaji wa pikipiki hizo.
Akizungumza na vyombo vya habari katika Makao Makuu ya Polisi Madema, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Mchomvu, amesema operesheni hiyo imelenga kudhibiti matukio ya wizi wa pikipiki yanayofanywa kwa njia ya uviziaji, hasa katika maeneo ya makaburini, misikitini, nyumba za ibada na nje ya makazi ya watu.
Kamanda Mchomvu ameeleza kuwa mtandao huo wa kihalifu unajumuisha makundi mawili, Kundi la kwanza linahusisha watu 12, ambapo 10 ni wezi wa pikipiki na wawili wanahusika kununua pikipiki hizo za wizi, Kundi la pili linahusisha watu watano ambao kazi yao ni kununua pikipiki hizo, kuzipeleka kwa mafundi ili kuondoa alama za utambulisho kama chassis number na kuzipa muonekano mpya, kabla ya kuziuza katika maeneo mbalimbali ndani ya Jiji la Zanzibar.
Aidha, Kamanda Mchomvu amewataka wananchi kuwa makini wanaponunua vyombo vya moto kwa kuhakikisha wanazingatia taratibu za usajili na umiliki halali, ili kuepuka kununua mali za wizi.
Amesema katika operation hiyo pikipiki 23 zimekamatwa na zinashikiliwa katika vituo vya Polisi vya Bububu na Madema.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliopoteza pikipiki zao wametoa shukrani kwa Jeshi la Polisi kwa juhudi wanazozichukua, ambazo zimewezesha kupatikana kwa baadhi ya pikipiki zilizokuwa zimeibwa.
Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shillah, ameeleza kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unafanyika kwa amani, utulivu na haki kwa wote.
Amesema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kupiga kura kwa amani na kuendelea na shughuli zake bila bughudha,. Kamanda Shillah amewataka wananchi kutoa taarifa mapema kwa vyombo vya dola pindi wanapobaini viashiria vya uvunjifu wa amani, na amewashauri kufuatilia ratiba zitakazotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ili kushiriki kikamilifu katika mchakato huo wa kidemokrasia.