Zenj FM
Zenj FM
13 October 2025, 4:34 pm

Mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir, amesema mpango wa kutoa posho ya shilingi 500,000 kwa kila Mzanzibari kila mwezi si ndoto bali ni dira inayotekelezeka kwa kupanga vipaumbele vya maendeleo na kutumia rasilimali za nchi kwa ufanisi.
Akizungumza na waandishi wa habari , Kikwajuni, Mjini Magharibi Unguja, Ameir amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kuinua hali ya maisha ya wananchi na kuhakikisha kila Mzanzibari anaishi maisha bora na yenye heshima
Akielezea Mikakati ya Utekelezaji ili kufanikisha dira hiyo, amesema Serikali ya Chama cha Demokrasia Makini itajikita katika kukuza uchumi kupitia sekta zenye tija kama Utalii kwa Kuboresha utalii wa kiutamaduni, kiikolojia na kihistoria, Kilimo kwa Kuboreshwa kwa miundombinu ya umwagiliaji,na ugawaji wa pembejeo bora bure kwa wakulima.
Amesema Chama cha Demokrasia MAKINI kimejipanga kuongeza mapato ya taifa kwa, Kuimarisha usimamizi wa rasilimali za nchi, kwa Kupambana na matumizi yasiyo ya lazima, pamoja na Kuwekeza kwenye maeneo yatakayoongeza pato la taifa kwa haraka.
Aidha mgombea hiyo ameahidi kutunga sheria mpya kali dhidi ya Wizi wa Fedha za Umma ambapo Wizi wa fedha za umma utachukuliwa kuwa uhalifu wa uhaini na adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 15 pamoja na kufilisiwa mali zoto na Viongozi watakaopatikana na hatia hawataruhusiwa kushika madaraka tena.