Zenj FM
Zenj FM
30 September 2025, 10:31 pm

Na Mary Julius.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jaji George Joseph Kazi, amesema jumla ya watu 8,325 wameondolewa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura baada ya kubainika kuwa hawana sifa, wakiwemo waliothibitishwa kufariki dunia.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud, Jaji Kazi amesema hatua hiyo inalenga kuboresha usahihi wa daftari na kuhakikisha linawiana na hali halisi ya sasa.
Amesema wapiga kura wote wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao wa 2025 ni 717,557.
Aidha, jumla ya vituo vya kupigia kura elfu nne mia nne na saba 4,407 pamoja na vituo vidogo elfu moja miasaba hamsini na mbili 1,752 vitatumika.
Kuhusu kura ya mapema, Tume imetenga maeneo 50, ambapo kila jimbo litakuwa na kituo kimoja maalum kwa lengo hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Thabiti Idarous Faina, amesema tume imefunga rasmi shughuli zote za uandikishaji wa daftari, ikiwemo uhamisho, masahihisho ya taarifa na kufutwa kwa wapiga kura waliopoteza sifa, ambazo zilikuwa zikifanyika katika ofisi za wilaya.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Aziza Iddi Suwed, amesema taarifa hiyo itasaidia kuongeza uwazi na kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Aidha Amewataka wadau kushirikiana kwa karibu na kuhamasisha jamii ili kila mwenye sifa ya kupiga kura afanye hivyo kwa amani na utulivu.
Wakitoa maoni yao baadhi ya wadau wa uchaguzi wameiomba Tume kuendelea kushirikisha pande zote katika kila hatua ya mchakato, huku waangalizi wa vyama vya siasa wakitaka kupewa muongozo maalum utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa uhuru na kwa mujibu wa sheria na taratibu.