Zenj FM

UPDP yaja na sera za afya bure na uvuvi bahari kuu

24 September 2025, 10:36 pm

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha UPDP, Hamad Mohammed Ibrahim Akizungumza katika mkutano  wa kampeni za chama hicho uliofanyika katika eneo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Na Mary Julius.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha UPDP, Hamad Mohammed Ibrahim, amesema endapo chama chake kitachaguliwa na kuingia madarakani kitadumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza katika mkutano  wa kampeni za chama hicho uliofanyika katika eneo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hamad amesema  Muungano umeleta manufaa makubwa kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo kuimarisha mshikamano na muingiliano wa kijamii kiuchumi kati ya Tanganyika na Zanzibar hasa kwa wakazi wa eneo hilo la Nungwi.

Mgombea huyo ametoa wito kwa wanachama na wananchi kwa ujumla kuwachagua viongozi watakaodumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akisisitiza kuwa chama chake kimejipanga kuulinda na kuuendeleza Muungano huo.

Aidha ameahidi kuendeleza sera ya afya bure kwa kote kwa kuongeza vifaa tiba pamoja na kuongeza wataalamu wa afya ili wananchi wapate huduma za afya za uhakika na salama.  

Sauti ya Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha UPDP, Hamad Mohammed Ibrahim.

Kwa upande wake, Mgombea Mwenza wa Urais kupitia chama cha UPDP Abdalla Mohamed Khamis amesisitiza umuhimu wa amani na utulivu, ametoa tahadhari dhidi ya wanasiasa wanaopotosha wananchi au kuhusika na vurugu kwa maslahi yao binafsi.

Sauti ya Mgombea Mwenza wa Urais kupitia chama cha UPDP Abdalla Mohamed Khamis

Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa UPDP, Abdul Bariki Ali Omar, amesema  chama hicho kimejipanga kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta ya uvuvi kwa kutoa vifaa vya kuvulia bahari kuu.

 Ametangaza mikakati ya chama ni pamoja na kuwekeza katika sekta ya utalii, na viwanda  ili kufanikiwa katika sekta hizo chama kitajenga vinu viwili  vya nyuklia Unguja na Pemba ili kuzalisha umeme wa kutosha kwa maendeleo ya viwanda visiwani Zanzibar.

Sauti ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa UPDP, Abdul Bariki Ali Omar.