Zenj FM

Mgombea urais Zanzibar kupitia NRA aahaidi mishahara minono kwa walimu

20 September 2025, 3:03 pm

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha NRA Khamis Faki Mgau akizungumza na wananchi wa Kangagani Mkoa wa Kaskadini Pemba katika mkutano wa hadhara wa kampeni..

Na Is-haka Mohammed.

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama cha NRA Khamis Faki Mgau amesema kuwa akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atapandisha mishahara ya waalimu ambapo walimu wa ngazi ya cheti ataanza kupokea kima cha mshahara wa shilingi milioni moja na laki tano(1,500,000).
Mgombea huyo wa Urais ameyasema hayo wakati akiwahutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara na wa ufunguzi wa kampeni kwa chama hicho uliofanyika huko Kangagani Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema pamoja na nyongeza hiyo kwa ngazi ya cheti, pia atapandisha mishahara kwa ngazi nyengine za elimu kwa walimu wa Unguja na Pemba na kusisitiza endapo atapewa ridhaa na wananchi jambo hilo ni rahisi kwa serikali atakayoingoza.

Sauti ya Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama cha NRA Khamis Faki Mgau.

Akizungumza katika Mkutano huo Mgombea Mweza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Khamis Ali Hassan amesema amewaomba wananchi wachague wagombea wanaotokana na chama hicho kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Urais wa Zanzibar,Wabunge, Wajumbe wa Bazara la Wawakilishi na Madiwani kwani wamesemamisha watu imara.

Nae Mgombea Uwakilishi wa Jimbo la Kojani ambae pia ni Naibu Katibu Mkuu wa NRA Khalid Makame Issa ameeleza kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake akichaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo hilo ni kuwawesha wakulima, wavuvi na wajasiriamali wa jimbo hilo ili kufanya shughuli hizo kwa weledi na kuongeza tija katika uzalishaji.

Sauti ya Mgombea Uwakilishi wa Jimbo la Kojani ambae pia ni Naibu Katibu Mkuu wa NRA Khalid Makame.