Zenj FM
Zenj FM
15 September 2025, 9:50 pm

Na Mary Julius,
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ADA-TADEA, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho Juma Ali Khatibu amesema dhamira ya chama chake ni kuendelea kuiunga mkono serikali iliyopo madarakani kutokana na kazi nzuri inayofanywa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.
Ameyasema hayo wakati akizindua rasmi kampeni za chama hicho kwa upande wa Zanzibar katika viwanja vya Magirisi, Fuoni Wilaya ya Magharibi B, amesema chama cha ADA-TADEA kimejipanga kuchukua nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ili kupata fursa ya kumshauri Rais katika masuala muhimu ya kitaifa.
Amesema endapo atapata ridhaa ya wananchi na kushika nafasi hiyo, atatoa mchango katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha elimu bora inatolewa kuanzia ngazi ya chekechea, kwa lengo la kukuza ubunifu kwa watoto.
Aidha, ameahidi kumshauri Rais kuhusu uwekezaji wenye tija katika sekta ya uvuvi , ili kuhakikisha vijana wanapata ajira endelevu kupitia shughuli hizo za baharini, jambo ambalo litaongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ADA-TADEA, George Bussungu, amesema chama hicho kimejipanga kuleta “Mapinduzi ya Njano”, yanayolenga kuondoa utegemezi wa kiteknolojia kwa kutumia mbinu za kisasa.
Aidha Ameahidi kutoa huduma ya Wi-Fi bure kwa kila Mzanzibari na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza uchumi wa ndani kwa kutengeneza bidhaa ndani ya Zanzibar.
Naye Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa ADA-TADEA Zanzibar, Ali Makame Isaa, ameahidi kugawa gesi kilo 20 kwa kaya maskini kila mwezi , kama sehemu ya kupunguza gharama za maisha na kulinda mazingira kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Aidha Ametoa wito kwa wanasiasa wote kuzingatia maadili ya kisiasa wakati wa kampeni na kuonya dhidi ya matumizi ya lugha za kibaguzi, akiiomba Tume ya Uchaguzi kufuatilia kwa karibu mienendo ya kampeni za vyama mbalimbali.